Thursday, April 21, 2022

Mbunifu Wa Kuyeyusha Chuma Asiyejua Kusoma Wala Kuandika Aomba Kupelekwa China Kupata Utaalamu

Shughuli ya uchomeleaji zana ikiendelea katika karakana ya Mzee Kisangani kwa vijana waliopata fursa ya ajira kupitia ubunifu wake.
Mzee Kisangani akizungumzia shughuli zake za utafiti alipotembelewa na waandishi wa habari katika eneo lake la kuyeyusha chauma.

Na Amiri Kilagalila,Njombe
Reuben Mtitu maarufu kwa jina la mzee Kisangani ambaye ni mbunifu na mtafiti wa kuyeyusha Chuma katika eneo la Mkiu wilaya ya Ludewa mkoani Njombe,ameiomba serikali kumsaidia ili aweze kufika nchi zilizobobea katika uyeyushaji wa chuma ili kujifunza zaidi utaalamu kutokana na uwezo alionao.

Mjasiliamali huyu mwenye umri wa takribani miaka 60 anayefanya shughuli mbambali mkoani Njombe ikiwemo kilimo cha Parachichi,kutengeneza zana zinazotokana na Chuma pamoja na kuyeyusha chuma.Ametoa ombi hilo alipotembelelewa na waandishi wa habari katika eneo lake la kuyeyusha chuma lililopo wilayani Ludewa.

“Niombe serikali iweze kunipeleka nchi zilizobobea kwenye uyeyushaji wa vyuma nikaone angalau mara moja tu kuwa wao wamefikia wapi anagalau na mimi niweze kuanzia pale kwasababu kitu ninachofanya hapa sijatazama kwa mtu ni kitu ambacho nimebuni mwenyewe”alisema Kisangani

Aidha licha ya ombi hilo Mzee Kisangani ameishukuru serikali kupitia waziri wa madini Dotto Biteko kwa kumtembelea katika eneo lake miaka kadhaa iliyopita na kutoa ahadi kadhaa ambazo baadhi ya ahadi hizo ziliweza kutekelezwa.

Miongoni mwa ahadi zilizofikiwa ni makaa yam awe kwa ajili ya moto kutumia kuyeyusha chuma ambapo mzee huyo amesema licha ya kupata mkaa huo lakini pia ameweza kuufanyia utafiti zaidi.

“Mkaa huu ni mzuri sana lakini nimeufanyia utafiti zaidi,huu mkaa niligundua una moshi na aina fulani ya mafuta na ukiangalia mkaa wa wachina hautoi moshi ila huu una mosho nikafanya utafiti ili kuondoa moshi ili huu mkaa uweze kutumika hata viwanda vya ndani badala ya kununua kutoka china na nimefanikiwa kwa hiyo unaweza kutumika hata maeneo ya makazi”aliongeza Kisangani.

Ezekia Mtweve na Janeth Kawogo ni miongoni mwa wananchi wanaonufaika na ubunifu pamoja na ujasiliamali unaofanywa na mzee huyo wameshukuru ubunifu wake kwa kuwa wanaendelea kupata riziki pamoja na kutunza familia zao.

“Mimi nipo kwa Kisangani Smith Group na katika ubunifu wake ametusaidia sana kupata ajila kwasababu mzee huyu amebuni miradi mingi,mimi nina watoto 6 ninawalea kupitia miradi ya huyu mzee na kule nyumbani kwangu tayari nina mradi pia wa ufugaji wa Nguruwe”alisema Ezekia Mtweve

Miongoni mwa zana mbali mbali zinazotengenzwa na mzee huyu kupitia chuma ni pamoja na Nyengo,visu,Panga na Nyundo huku akiwa pia amesaidia vijana zaidi ya 400 kujifunza shughuli mbali mbali kupitia ubunifu wake na kwenda kuendeleza ujuzi wao katika maeneo mengine.

No comments :

Post a Comment