Monday, April 25, 2022

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA YAAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO KATIKA KIWANDA CHA ALAF LIMITED

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakipata maelekezo kutoka kwa mmoja wa Wataalamu wa kuendesha mitambo ya uzalishaji katika Kiwanda cha ALAF Limited kilichopo jijini Dar es Salaam.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mhe. David Kihenzile (Pichani) wakipata maelekezo kutoka kwa Mtaalamu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) katika Kiwanda cha ALAF Limited jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Maafisa wa Kampuni ya ALAF Limited.

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zinazoikumba Kiwanda cha ALAF Limited, sanjari na kusifu jitihada za uendeshaji na uzalishaji mzuri unaofanywa na Kiwanda hicho kilichopo nchini.

Akizungumza katika ziara hiyo ya kutembelea Viwanda vya ALAF na MMI Steel, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. David Kihenzile amesema wamejifunza mambo mengi ndani ya Kiwanda hicho ambapo ameeleza kuwa Serikali kupitia wao itahakikisha Kampuni hiyo inakuwa na mazingira mazuri ya kufanya kazi na hatimaye Taifa kupata Kodi kupitia Kiwanda hicho kama Mwekezaji.

Amesema lengo la nchi ni kuhamasisha Uwekezaji katika Mataifa mbalimbali duniani kuja kuwekeza Tanzania , ikiwa sambamba na vijana kunufaika na nafasi za ajira kupitia Wawekezaji hao hapa nchini. Hata hivyo amesema Serikali inahamasisha Wawekezaji wengine kutoka nchi mbalimbali kuja nchini kuwekeza kutokana na mazingira bora na utulivu kwa wageni.

“Sisi kama Watanzania tunatamani na tunafurahi kuona bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa hapa nchini zinaenda kuuzwa kwenye Mataifa na Jumuiya mbalimbali duniani”, amesema Mhe. Kihenzile.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Ashish Mystry amesema ujio wa Kamati hiyo unaonesha uwajibikaji mzuri wa Serikali katika kuhimiza uzalishaji wa Viwanda nchini, ikiwa sambamba na kuwaelezea changamoto za Kiwanda hicho ambapo Kamati hiyo kupitia Mwenyekiti, Wajumbe wake wameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kupata muafaka mapema na haraka iwezekanavyo.

Pia, Meneja Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi amesema ujio wa Kamati hiyo katika Kiwanda hicho, umewapa moyo kuwa Serikali ya Tanzania ipo pamoja na Wawekezaji wake wanaokuja kuwekeza nchini na kukuza dhana ya Tanzania ya Viwanda.

“Sisi kama ALAF tunafurahi kufikisha changamoto mbalimbali katika Kamati hii ya Bunge, tunaamini changamoto hizo zitafanyiwa kazi na sisi tunaendelea kusisitiza kwamba tupo pamaja na Tanzania kama Wawekezaji”, amesema Bayuni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MMI Steel, Patel Veer amesema endapo Serikali itashugulikia changamoto za bidhaa bandia na kuweka mazingira sawa kwa wafanyabuashara wote, sekta hiyo itakuwa kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

No comments :

Post a Comment