Thursday, March 31, 2022

OPERESHENI ANWANI ZA MAKAZI SASA NI ASILIMIA 67


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati wa mkutano na Wakuu wa Mikoa uliofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza wakati wa mkutano na Wakuu wa Mikoa uliofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi.



Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na Wakuu wa Mikoa na viongozi mbalimbali katika mkutano wa Wakuu wa Mikoa kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi jijini Dodoma.



Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiagana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa baada ya mkutano wa wakati Wizara hizo na Wakuu wa Mikoa wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi uliofanyika jijini Dodoma.

************************

Operesheni ya uwekaji wa Anwani za Makazi nchini iliyotangazwa tarehe 8 Februari mwaka huu wa 2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 67 kulingana na takwimu za mfumo unaopokea taarifa za utekelezaji wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye wakati wa mkutano na Wakuu wa Mikoa yote nchini uliofanyika jijini Dodoma uliolenga kutoa taarifa ya utekelezaji wa operesheni hiyo.

“Tathimini iliyofanyika ya kupata asilimia 67 imezingatia kazi zilizotekelezwa ikiwa ni kazi ya kutambua maeneo; kujenga uwezo kwa maafisa na watendaji wanaofanya kazi hii; kutoa elimu ya zoezi husika; kukusanya taarifa; kutengeneza mfumo utakaopokea taarifa na kuingiza taarifa kwenye mfumo ili ziweze kutumika na kuweka muundombinu (physical) katika maeneo mbalimbali nchini”, amezungumza Mhe. Nape.

Ameongeza kuwa mwenendo wa utekelezaji unaonesha matumaini ya zoezi kukamilika kabla ya muda uliopangwa na kazi itakayofuata itakuwa ni kusafisha baadhi ya taarifa kwenye mfumo kwa hatua za kuukabidhi mfumo kwa mujibu wa maelekezo ya kuukabidhi ifikapo tarehe 22 Mei, mwaka 2022.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Wizara anayoisimamia kwa pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni timu ya ushindi na wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha wanasimamia ipasavyo maelekezo ya Mhe. Rais ya kukamilisha operesheni ya Anwani za makazi mwishoni mwa mwezi Mei, 2022

“Nisisitize kuwa asilimia 67 zilizofikiwa ni hatua nzuri lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, sina shaka na Wakuu wa Mikoa, ujenzi wa madarasa ya mama Samia mlifanya vizuri hivyo naamini na hili operesheni ya Anwani za Makazi mtafanya vizuri”, Amezungumza Bashungwa

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa, Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa nchini, Mhe. John Mongella Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa operesheni hiyo inaendelea vizuri na itakamilika kwa muda uliopangwa

Aidha, ameishukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutoa wataalamu kwenda kusaidia utekelezaji wa operesheni hiyo pale panapohitajika ili kuongeza ufanisi hasa kwenye mikoa yenye maeneo makubwa na idadi kubwa ya watu. Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameitisha mkutano huo kwa lengo la kujadili namna wakuu wa mikoa wanavyoendelea kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya operesheni maalumu ya Anwani za makazi nchini ambayo imeunganika na maandalizi ya sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu

No comments :

Post a Comment