Tuesday, February 22, 2022

Makandarasi Nchini Watakiwa Kukamilisha Miradi Kwa Wakati.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabrieli, katikati, akizungumza na wakandarasi Wazalendo wanaotekeleza miradi mbali mbali ya mahakama wakati wa kikao chake cha kufahamiana na wakandarasi hao kilichofanyika leo Februari 22,2022 katika kituo Jumuishi, Kinondoni jijini Dar es Salaam.  Kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufaa, Solanus Nyimbi na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu,  Leonard Magacha.
Baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi mbali mbali ya Mahakama, wakimsililiza Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante Ole Gabrieli, katikati, wakati wa kikao chake cha kufahamiana na wakandarasi hao kilichofanyika leo Februari 22,2022 katika kituo Jumuishi, Kinondoni jijini Dar es Salaam.Na Karama Kenyunko Michuzi TV

MTENDAJI Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel amewataka makandarasi wazalendo wanaofanya miradi ya mahakama kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati huku ikiwa na ubora wa viwango vinavyotakiwa.

Amesema, kukamilika kwa miradi hiyo kutaiwezesha mahakama pia kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Profesa Ole Gabrieli ameyasema hayo leo Februari 22, 2022 wakati wa kikao chake na makandarasi wa miradi ya mahakama katika Kituo Jumuishi cha Kinondoni, Dar es Salaam

Amesema, mpaka sasa mahakama ina miradi 34 inayoendelea katika mikoa mbalimbali na imewaamini wakandarasi wa ndani kufanya kazi katika miradi hiyo, hivyo watumie fedha watakazopatiwa kwa matumizi sahihi.

"Tuna Mahakama za Mwanzo 960, Mahakama za Wilaya 120, Mahakama za Hakimu Mkazi 30, Mahakama Kuu 18 na Rufani lakini pia tuna vituo vya kutolea huduma sita katika Mikoa mitano na ujenzi unaendelea," amesema Profesa Gabriel.

Amesema, lengo kubwa kutumia makandarasi wa ndani ni kuwakuza katika kazi zao hivyo, wanapaswa kuongeza kasi ya utendaji na utaalamu.

"Mahakama inampango wa kuona kuwa inawakuza wakandarasi wa ndani na ndio maana sisi kama mhimili tunashirikiana na taasisi zingine kuhakikisha kuwa hata hizi kazi za ujenzi zinakwenda vizuri ikiwepo ERB na zinginezo" amesema.

Aidha, aliwataka wakandarasi hao kuwa imara kifedha kwa sababu upatikanaji wa fedha serikalini unahitaji mchakato hivyo, wasisubiri fedha ndipo waanze ujenzi badala yake waendelee na ujenzi na wakati wakisubiri kulipwa fedha zao

Pia amesisitiza kuwa serikali ina mpango wa kuwapatia fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi mingine kwa hiyo wakandarasi hao watumie dhamana waliyopewa ili wawafikirie kwa miradi ijayo.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya ujenzi ya United Builders, Anold Kileo ameisema mkutano huo umekuwa wa faida kwao kwani umewapa ushawishi wa kufanya kazi kwa nguvu zaidi.

"Sisi kama wazawa tunafanya bidii ili tunachopata tunakifanyia kazi nzuri lengo tuendelee kuaminika kupewa kazi zaidi na pia ametuahidi kuna kazi nyingi zinakuja, kwa hiyo tutaenda kuchapa kazi kwa nguvu," alisema Kileo.

Amesema amepewa miradi ya ujenzi wa mahakama katika Mikoa ya Mara na Simiyu ambapo anajenga mahakama za wilaya, jengo kubwa la mahakama, jengo la choo cha nje, jengo la walinzi, mashimo ya choo na mashimo ya maji ya mvua.

Amesema, kampuni yake inaahidi kuendelea kufanya kazi kwa nguvu zote na kwamba miradi aliyopewa haipo kwenye hatari ya kuchelewa kwani wanamtegemea kukamilisha miradi hiyo Aprili mwaka huu.

No comments :

Post a Comment