Na Christian Gaya-HakiPensheni Center
Maamuzi haya yalitolewa ni ya kufuatana na Kamati hiyo iliyofanya kikao
chake cha kawaida cha 218 tarehe 31 Januari 2022, na kupitia utekelezaji wa
sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia.
Aidha, Kamati imeridhishwa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara, uliokua kwa wastani wa asilimia 4.9 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2021.
“Ukuaji huu umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchimbaji
madini, viwanda na usafirishaji. Aidha, Kamati ilibaini ongezeko la mfumuko wa
bei kufikia asilimia 4.2 mwezi Desemba 2021 kutoka asilimia 3.8 mwezi Julai
2021, kutokana na changamoto za ugavi, hata hivyo mfumuko wa bei unatarajiwa
kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5. Uchumi wa Zanzibar umekua kwa
kasi ya kuridhisha kufikia asilimia 8.8 katika robo ya tatu ya mwaka 2021,
ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho 2020, kutokana na
kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, hususan utalii. Mfumuko wa bei uliongezeka
kidogo, ukichangiwa na bei zisizo za vyakula, hata hivyo umeendelea kubaki
ndani ya lengo la chini ya asilimia 5,” Gavana Benki Kuu ya Tanzania, Profesa
Florens Luoga anasema.
Anasema Kamati imeridhishwa na kuimarika kwa ukuaji wa
mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 7.8 na asilimia 10 mwezi Novemba na
Desemba 2021, mtawalia, kutoka chini ya asilimia 5 kwa sehemu kubwa ya mwaka
2021. Mwenendo huu ni sambamba na lengo la ukuaji wa asilimia 10.6 kwa mwaka
2021/22. Ukuaji huu ulichangiwa na utekelezaji wa sera ya fedha yenye kuongeza
ukwasi katika uchumi; utekelezaji wa hatua za ziada za kisera zinazolenga
kuchochea utoaji wa mikopo na kushusha viwango vya riba; pamoja na kuimarika
kwa shughuli za kiuchumi kufuatia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia.
Sekta ya nje imeendelea kuimarika kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19,
ikidhihirishwa na kurejea kwa shughuli za utalii.
Profesa Luoga anaeleza ya kuwa akiba ya fedha za kigeni
ilifikia dola za Marekani bilioni 6.4, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na
huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 6.6. Utekelezaji wa bajeti ya Serikali
uliendana na matarajio kutokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na
misaada na mikopo kutoka nje.
“Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa ndani pamoja na wa dunia, na hivyo matarajio ni kuwa malengo ya sera ya fedha yaliyowekwa katika Tamko la Sera ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2021/22 yatafikiwa,” Gavana Luoga ambaye ndiye mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania anasisitiza.
No comments :
Post a Comment