Wednesday, February 2, 2022

EWURA yatoa muelekeo wa bei mpya za mafuta kwa mwezi Februari, 2022


Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma.

MAMLAKA ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA)imetoa bei mpya za mafuta ya taa,petroli na dizeli kuanzia Februari 2,2022 huku baadhi ya Mikoa ikipanda na mingine ikipungua.

Bei hiyo imetolewa jijini hapa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Mhandisi Godfrey Chibulunje,wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa bei za mafuta nchini ambazo hutangazwa kila mwanzo wa mwezi..

Amesema bei za rejareja za mafuta ya taa,dizeli na petroli yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar Es Salaam zimepungua kwa shilingi 21/Lita (Petroli), Shilingi 44/lita wakati bei ya dizeli ikiongezeka Kwa shilingi 13 kwa lita.

Amefafanua kuwa bei za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini ambayo ni Tanga, Kilimanjaro,Arusha na Manyara zimepungua kwa shilingi 123 kwa lita ya petroli na shilingi 92 kwa lita ya Dizeli.

“Kutokana na kumalizika kwa mafuta ya taa kwenye maghala ya kuhifadhia yaliyopo Tanga,waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka bandari ya Dar Es Salaam,”amesema.

Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo wa EWURA ameeleza kuwa bei za rejareja za mafuta ya taa kutoka mikoa hiyo ya Kaskazini itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia bandari ya Dar Es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.

Pamoja na hayo Chibulunje alieleza mwenendo wa bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kusini ikihusisha Mtwara, Lindi na Ruvuma zitaendelea kuwa zile zile zilizotangazwa katika toleo la Serikali la tarehe 5, Januari ,2022 kutokana na sababu kwamba Kwa mwezi Januari 2022 hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

“Pia kwa kuwa hakuna maghala ya kuhifadhia mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara,waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kusini tunawashauri kuchukua mafuta ya taa kutoka bandari ya Dar Es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia bandari hiyo,”amefafanua Chibulunje.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo ameeleza mwenendo wa bei za mafuta kwa mwezi Machi na Aprili mwaka huu kwa kufuatilia bei za soko la dunia,na kusema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa bei za mafuta.

“EWURA itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta kwa ukaribu ili kuona namna ya kuishauri Serikali hatua za kuchukua katika harakati za kupunguza makali ya bei,”amesema.


No comments :

Post a Comment