Wednesday, February 2, 2022

Corona Ilivyoleta Athari Kwa Wanasheria



Chama cha wanasheria wa Tanganyika  TLS mkoa wa Njombe kimesema tangu kuanza kwa ugonjwa wa Uviko 19 mawakili 65 nchini wamefariki dunia pamoja na kuathiri hali ya kiuchumi.

Hayo yameelezwa na mratibu wa chama cha wanasheria Tanganyika TLS mkoa wa Njombe  Innocent Kibadu katika maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika viwanja wa mahakama  ambapo alisema athari za uviko hazikuishia tu kuchukua maisha ya wapendwa wao bali tu imeathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kiuchumi kwa mawakili binafsi na familia zao.

"Athari za uviko 19 ni nyingi ikiwa ni pamoja na watu kupoteza maisha,kudhoofika mwili,kupunguza kasi ya kufanya kazi, kuathiri uwezo wa taasisi mbalimbali zinazojitegeme na za umma kujiendesha kiufanisi na kurudisha nyuma mipango ambayo kila taasisi imejiwekea"alisema Kibadu.

Kibadu aliongeza kuwa"sisi kama chama tumepoteza jumla ya mawakili wenzetu wapatao 65"alisema.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe Marwa Rubirya,mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa alisema jamii inapaswa kujitokeza kupata chanjo ya Uviko 19 kwa sababu ni salama kwa binadamu.

"Chanjo ipo kwenye vituo vyote vya kutokea huduma,chanjo hii ni salama nendeni mkachanje ili muweze kuwa salama"alisema Kasongwa.

Naye hakimu mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Njombe Liadi Chamshama amesema kuwa uanzishwaji wa mahakama ya kimtandao itasaidia kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani.

"Licha ya kupunguza mrundikano wa watu pia itasaidia ufanisi na kupunguza uwapo wa mashauri mengi yanayoletwa mahakamani kwa mujibu wa sheria"alisema Chamshama.

No comments :

Post a Comment