Friday, February 25, 2022

BASHE AVUTIWA NA WAWEKEZAJI WAKUBWA KUWEKEZA KILIMO NCHINI

Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe akizungumza na mtoto wa mtawala wa Dubai, Sheikh Ahmed Dalmook Al Maktoum ambapo wamejadiliana mikakati mbalimbali ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini. Familia hiyo ya kifalme inamiliki kampuni kubwa za biashara ya kilimo yenye mtandao dunia nzima, Bashe yupo Dubai kwenye Maonesho ya biashara ya kimataifa ambapo amezitangaza fursa za kilimo zinazopatikana hapa nchini.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akijadiliana na Mkuu wa Taasisi ya Agra(kushoto) na Mwakilishi wa Agra Jenifer Bani katika kikao cha Mawaziri wa Kilimo Dubai hivi karibuni.

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kampuni kubwa duniani kuwekeza kwenye kilimo ili kukiongezea thamani na kuhakikisha usalama wa chakula kwa miaka mingi ijayo.

Akihutubia kwenye Maonesho ya Biashara Kimataifa ya (Dubai Expo,) yanayoendelea katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu, Bashe alibainisha kuwa Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba kwa uwekezaji wa kilimo huku mazingira ya uwekezaji yakiwa ya kuvutia uwekezaji katika kila aina ya kilimo.

Aidha Bashe amesema, kwa sasa nchi inatafuta wawekezaji wa kimkakati ambao watasaidia uwekezaji wenye tija kwa Tanzania na dunia kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa kwa miaka ijayo Afrika ndiyo itakuwa chanzo kikubwa cha chakula.

“Tanzania inawapenda na kuwatambua wawekezaji katika sekta zote hasa za kilimo kwa kuwa ni sekta ambayo ipo na itaendelea kuwepo miaka yote kwa kuwa chakula ni kitu muhimu ambacho bado kinahitajika kwa mustakabali wa mwanadamu kuendelea kuishi, labda wanasayansi waje na utaalamu wa kuweka chip mwilini ili mtu akiamka asisikie njaa” amesema Bashe.

Kutokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kupunguza riba za benki hadi kufikia kuwa chini ya asilimia 10 kuwavutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi, ni fursa kubwa kwa wawekezaji hao kujikita kwenye kilimo kwa kuwa mazingira ni rafiki zaidi.

 Tanzania inajulikana kimataifa kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo ina vyeti vya utambulisho wa kimataifa ambavyo vinawawezesha wawekezaji hao kuuza bidhaa kimataifa kutoka Tanzania.

"Nchi ina vituo vingi vya utafiti wa kilimo vilivyosambaa kila kona ya nchi ambapo vinafanya utafiti wa aina ya mazao yanayopaswa  kulimwa katika eneo husika, pia nchi ina nguvu kazi ya kutosha ya kufanya kazi kwenye mazingira yoyote ya uwekezaji huku pia kukiwa na motisha nyingi kwa ajili ya wawekezaji sasa nchi ipo tayari kufanya kazi na wawekezaji katika kilimo hasa ikizingatiwa ardhi ipo ya kutosha.”

Alitolea mfano wa kampuni ya AvoAfrika ambayo imesafirisha kontena zaidi ya 200 za parachichi kutoka Tanzania huku akibainisha kuwa kwa sasa hapa nchini kilimo ni biashara na siyo sehemu tu ya kujipatia mlo huku akibainisha kuwa Dubai inachukuliwa kati ya sehemu muhimu kwa kuuza mazao ya kilimo kutoka Tanzania.

Kwa upande wa kilimo cha matunda na mbogamboga Tanzania inasifika kwa kuwa na uwezo wa kuzalisha aina zote za matunda na mbogamboga huku fursa zikiwa nyingi za kuuza ndani na nje ya nchi huku akifafanua zaidi kuwa hapa nchini kuna mazingira mazuri ya kilimo cha umwagiliaji.

 Licha ya kuwaalika wawekezaji kutoka nje ya nchi bado wizara yake inaendelea kuwathamini na kuwaendeleza wakulima wadogowadogo na imeshawawezesha kunufaika na mikopo ya aina mbalimbali kama ilivyo kwa wajasiriamali wengine wadogowadogo.

No comments :

Post a Comment