Sunday, January 2, 2022

Rais Dkt.Mwinyi awasili Pemba kwa ziara ya kikazi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na viongozi wa Serikali alipowasili Uwanja wa Ndege wa Chakechake Pemba akiwa katika ziara ya kikazi ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar,kwa ajili ya kuzindua Miradi ya Maendeleo kisiwani Pemba kesho Januari 3,2022.(Picha na Ikulu).

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewasili kisiwani Pemba leo kwa ziara ya kikazi ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. 

Awali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Rais Dkt.Mwinyi aliagwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah ambapo baada ya kuwasili kisiwani humo akiwa amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi alipokewa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahor Masoud. 

Akiwa kisiwani Pemba, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kesho Januari 3,2022 mapema asubuhi anatarajiwa kushiriki katika ufunguzi wa Matembezi ya Vijana wa UVCCM Zanzibar huko Konde, Mkoa wa Kaskazini Pemba. 

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi baada ya shughuli hiyo anatarajiwa kuwasili Kinyasini Wete kwa ajili ya kuweka jiwe la Msingi Kiwanda cha kutengeneza Maji Safi Watercom (T) Ltd na baadae kuwahutubia wananchi.

No comments :

Post a Comment