Thursday, December 30, 2021

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) larekodi mafanikio ya kihistoria 2021


NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limefanikiwa kurekodi mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu nchini kwa mwaka huu wa 2021.

Hayo yamesemwa leo Desemba 30,2021 na Meneja wa Huduma na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi mbalimbali wa habari makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika, Dkt.Maulidi Banyani kuelezea mafanikio mbalimbali waliyoyapata kwa mwaka 2021 na matarajio yao mwaka ujao wa 2022.

"Tulipoanza mwaka 2021 tulikuwa na miradi 26 ya nyumba za gharama nafuu amnbayo ilikuwa bado haijakamilika katika mikoa ya Mtwara (Masasi), Katavi (Mlele),Tabora (Igunga) na Njombe (Makete), nichukue nafasi hii kuujulisha umma kuwa, tayari miradi yote imekamilika,"amesema Saguya.
Juhudi za Serikali kupitia NHC katika kutekeleza miradi ya nyumba za makazi za gharama nafuu sehemu mbalimbali nchini zinalenga kupunguza adha ya makazi kwa watumishi wa halmashauri na wananchi kwa ujumla.

Miradi mikubwa

Mbali na hayo, Meneja huyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa, shirika pia limeanza kutekeleza miradi minne mikubwa ya Morocco Square, Kawe 711, Golden Premier Residence (GPR) na Plot (Kitalu) 300 Regent Estate ambayo ilisimama tangu mwaka 2017 kutokana na upungufu wa fedha.

"Hivyo, katika kufanikisha ujenzi wa majengo hayo makubwa, shirika limepewa kibali cha awali na Serikali cha kukopa shilingi bilioni 44.7 ili kumalizia mradi wa Morocco Square na Plot 300 Regent Estate, baada ya hapo miradi miwili iliyobaki itafuatia.

"Aidha, pamoja na miradi yetu wenyewe ambayo tumekuwa tukiitekeleza sehemu mbalimbali nchini, pia tumepewa miradi mbalimbali ya kimkakati na Serikali ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo jumla ya miradi 17 yenye majengo 44 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 12.96 ilitekelezwa,"amebainisha Saguya.

Pia, NHC imejenga majengo ya ofisi ikiwemo ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa shilingi bilioni moja, ofisi za halmashauri za Malinyi mkoani Morogoro kwa shilingi bilioni 3.78 na Wanging'ombe mkoani Njombe kwa shilingi bilioni 2.7.

Kandarasi kubwa

Meneja huyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema kuwa, pamoja na miradi hiyo Serikali ililipatia shirika kandarasi ya kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusingi Mitengo mkoani Mtwara kwa shilingi bilioni 15.8, Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa mkoani Mara kwa shilingi bilioni 17.2 na machinjio ya kisasa ya Vingunguti mkoani Dar es Salaam kwa shilingi bilioni 15.2.

"Miradi hiyo imekamilika na imeanza kutumika, shirika pia limeweza kuimarisha maeneo ya mipaka yetu kwa kujenga majengo makubwa ya biashara likiwemo jengo la Mutukula Commercial Complex tulilolijenga katika mpaka wa Tanzania na Uganda, na sasa tuko katika mpango wa kujenga jengo kubwa la biashara katika mpaka wetu wa Tanzania na Kenya eneo la Kirongwe mkoani Mara,"amefafanua Saguya.

Dodoma

Wakati huo huo katika kusaidia suala la makazi baada ya Serikali kuhamia Dodoma, Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba za makazi 1,000 ambapo kwa mujibu wa Meneja huyo, awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 404 imekamilika katika eneo la Chamwino.

Amesema, nyumba 101 zitapangishwa kwa watu mbalimbali na nyumba 303 za makazi zimejengwa katika eneo la Iyumbu kwa ajili ya kuuzwa kwa wananchi.

"Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu nyumba za makazi zipatazo 325 zitajengwa, na awamu ya tatu itakuwa na idadi ya nyumba 275,"amebainisha Saguya.

Mbali na hayo amesema kuwa, shirika hilo pia limesaidia kujenga majengo makubwa ya taasisi mbalimbali za Serikali katika Jiji la Dodoma ikiwemo Ofisi ya Kanda ya Kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa shilingi bilioni 6.8

"Sanjari na hilo, shirika limeendelea kuaminiwa na Serikali kwa kupewa kandarasi ya ujenzi wa majengo nane ya wizara mbalimbali katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma (awamu ya pili). Miradi yote ina jumla ya shilingi bilioni 186.83,"amefafanua Saguya.

Usimamizi wa nyumba

Mkurugenzi wa Usimamizi Miliki na Masoko wa NHC, Elias Msese akizungumzia kuhusu usimamizi wa miliki wa nyumba zipatazo 18,622 amesema kuwa,shirika limebuni mpango wa matengenezo ya nyumba wa miaka mitano kuanzia 2021/22-25/26.
Amesema, katika kufanikisha hilo limetenga shilingi bilioni 8.5 kwa mwaka huu wa fedha ili kukarabati majengo yake 350.

"Shirika limeshaanza ukarabati wa baadhi ya majengo katika Mkoa wa Kilimanjaro na Dar es Salaam, ukarabati unaofanywa katika nyumba na majengo mengine utatumia zaidi ya shilingi bilioni 50 katika miaka mitano ijayo, huu ni ukarabati mkubwa utakaohusisha kubadilisha paa, vyoo na madirisha chakavu,"amebainisha.

Kampeni kabambe

Katika hatua nyinyinge shirika hilo limeanza kuyafanyia mapitio madeni ya kodi na kuyahakiki ili kubainisha kila mdaiwa na mahali alipo ili mwezi Januari, 2022 shirika lianze kampeni kabambe ya ukusanyaji madeni hayo.

Meneja wa Huduma na Uhusiano, Saguya amesema, hadi sasa NHC inadai malimbikizo ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 26 kutoka kwa wapangaji wake, hivyo shirika limeanza kufanyia mapitio madeni hayo na kuyahakiki.

Amesema, malimbikizo hayo yana uwezo wa kujenga nyumba nyingine 450 ambazo zitawasaidia watanzania wengine kupata makazi kupitia shirika hilo nchini.

“Mpaka sasa tumeshaanza mazungumzo na baadhi ya wadaiwa zikiwemo taasisi za serikali, kufikia Januari shirika litaanza mpango wa kukusanya madeni yake yote, hayo ni maelekezo ya Serikali na bodi kwa wapangaji wasio waaminifu,”amesema Saguya.

Pia amesema kuwa, shirika limebaini wapangaji wasio halali wanaoishi kwenye nyumba kinyume na utaratibu wapatao 30 na tayari wamewachukulia hatua za kisheria kwa kuwanyang’anya upangaji na kuwapatia wanaostahili.

Matarajio 2022

Meneja wa Huduma na Uhusiano, Saguya amesema kuwa, mwaka ujao shirika hilo linatarajia kutekeleza ujenzi wa majengo ya biashara ya Kashozi Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Mtanda mkoani Lindi, Kahama mkoani Shinyanga na Masasi mkoani Mtwara.

"Pia shirika litajenga nyumba za makazi Isomvu mjini Sumbawanga na maghala ya mazao sehemu mbalimbali nchini, shirika litaendelea na mradi wa uuzaji viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara katika eneo la Safari City Arusha.

"
Vile vile, shirika linatarajia kuanzisha viwanda vyake vya matofali, kokoto na mabati kwa ajili ya kupunguza gharama za ujenzi na kupata vifaa bora vya utekelezaji wa miradi yetu,"amefafanua Meneja huyo.

Meneja wa Huduma na Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu ameongeza kuwa, shirika hilo linatarajia mwakani kukusanya kodi na malimbikizo yote, "na tunatarajia kuwafikisha mahakamani watakaokaidi kulipa madeni yao,"amesema.

No comments :

Post a Comment