Wednesday, November 10, 2021

WCF IMESAJILI ASILIMIA 90 YA WAAJIRI WOTE NCHINI: DKT. JOHN MDUMA

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii (Ofisi ya Waziri Mkuu), Festo Fute wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2021.
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kulia), Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba (kushoto) wakimsikilzia Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii (Ofisi ya Waziri Mkuu), Festo Fute wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2021.
Maafisa wa WCF, wakimsikiliza mwananchi aliyetembelea banda la Mfuko huo Novemba 10, 2021
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF, Laura Kunenge kwenye banda la Mfuko wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2021.
Mwananchi(kushoto) akisikiliza kwa makini maelezo aliyokuwa akipewa na Afisa wa WCF
Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya TCB, Sabasaba Moshingi (kushoto) akipatiwa huduma na wafanyakazi wenye sura za bashasha wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Afisa Madai Mwandamizi, Silvanus Kuloshe (wapili kulia) na Sarah Reuben, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WCF kwenye banda la Mfuko huo kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya TCB, Sabasaba Moshingi (kushoto) akipokea chapisho lenye taarifa mbalimbali za WCF kutoka kwa Afisa Madai Mwandamizi wa Mfuko huo Silvanus Kuloshe

NA MWANDISHI WETU, MNAZI MMOJA, DAR

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema mpaka sasa Mfuko umeweza kusajili asilimia 90 ya waajiri wotenchini ambao wako kwenye kanzidata ya Mfuko

Dkt. Mduma ameyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ambapo WCF inashiriki kama taasisi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye jukumu la kulipa Fidia kwa Mfanyakazi aliyeumia, Kuugua au Kufariki kutokana na kazi kwa mujibu wa mkataba wa ajira.

“Tunaendelea kuwahimiza Waajiri waendelee kuwasilisha michango yao kwa wakati na Mfuko uendelee kulipa Mafao kadri ya wale wanaohitaji wanavyojitokeza.” Alifafanua.

Alitoa wito kwa wadau wa Mfuko ambao ni Waajiri waendelee kushirikiana na Mfuko kama inavyopasa  lakini pia wadau wengine ambao ni wale wanaopata Mafao, amewahakikishia kuwa Mfuko wao uko imara na unaendelea kutoa Mafao kwa Mujibu wa Sheria.

Akizunhumzia ushiriki wa Mfuko kwenye Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, Dkt. Mduma alisema “ Sekta ya Hifadhi ya Jamii ni moja ya Sekta pana ya Fedha na WCF ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wenye jukumu la kulipa wafanyakazi wanaoumia, kuugua au kufariki kutokana kazi.

Alisema katika kufanya jukumu hilo Mfuko unashiriki katika shughuli za Uwekezaji kwa michango inayokusanywa inawekezwa kwenye maeneo mbalimbali.

“Utaona kwamba Mfuko unaingia kwenye sekta ya fedha katika Nyanja mbili ya kwanza kuratibu michango kama sekta ya hifadhi ya jamii lakini pia fedha zinazopatikana zinawekezwa na kwa kufanya hivyo tunashiriki katika sekta pana ya fedha.” Alisema Dkt. Mduma.

Kwa mujibu wa waandaaji wa maadhimisho hayo, Wizara ya Fedha na Mipango, walengwa wakuu wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo: watumishi wa umma; wanafunzi; wakufunzi; wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu; wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs); asasi za kiraia; Wahariri na waandishi wa vyombo vya habari; watoa huduma za fedha; na umma kwa ujumla.

Lengo la Maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 8 na yanatarajiwa kufikia kilele Novemba 14, 2021 ni kuhakikisha Umma wa Watanzania unaelewa vema fursa zilizopo kwenye sekta ya fedha, ili kuinua vipato vyao na hatimaye kukuza uchumi wa taifa.

No comments :

Post a Comment