Tuesday, November 30, 2021

SEKTA ZA MIFUGO SMT NA SMZ ZAWEKA MIKAKATI YA MAENDELEO


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amosy Zephania akifungua rasmi kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa Sekta za Mifugo kilichofanyika Chakechake Pemba ambapo kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha wataalamu . Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Maryam Juma Sadallah. 


Baadhi ya wataalam walioshiriki kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa Sekta za Mifugo wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo (Mifugo) Bw. Amosy Zephania (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho kilichifanyika Chakechake Pemba 


Baadhi ya wataalam walioshiriki kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa Sekta za Mifugo wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo (Mifugo) Bw. Amosy Zephania (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho kilichifanyika Chakechake Pemba. 


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Amosy Zephania (wa pili kulia) akieleza dhamira ya ushirikiano wa Serikali mbili (SMT na SMZ) kuwa ni kutatua changamoto za wafugaji nchini kwa mfugaji bora wa ng’ombe Bwana Ahmed Shabaan Salum (kulia kwake)!walipomtembelea shambani kwake eneo la Kinyasini Wilaya ya Wete Pemba. 


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Amosy Zephania (kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar Bi. Maryam Juma Sadallah wakiongea na mfugaji (hayupo pichani )mara baada ya kukagua banda la kufugia ng’ombe la Bwana Ahmed Shabaan walipomtembelea shambani kwake eneo la Kinyasini Wilaya ya Wete Pemba. 


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo, na Ugani Dkt. Angello Mwilawa (aliyeshika majani) na baadhi ya wataalam walioshiriki kikao cha ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa Sekta za Mifugo wakikagua malisho kwa mfugaji bora wa ng’ombe Bwana Ahmed Shabaan Salum walipomtembelea shambani kwake eneo la Kinyasini Wilaya ya Wete Pemba. 

.......................................................... 

Sekta za Mifugo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia makatibu wake wakuu wamekutana na kuweka mikakati ya kuendeleza sekta hizo kwa wafugaji wa pande mbili za Muungano ambapo maazimio saba yameridhiwa ikiwa ni hatua ya kufikia malengo tarajiwa. 

Maazimio hayo yamefikiwa Wilayani Chakechake Pemba, kwenye kikao kilichowakutanisha makatibu wakuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT)wa Sekta ya Mifugo Bw. Amosy Zephania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Bi. Maryam Juma Sadallah. Akifungua rasmi kikao hicho Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo (SMT) Bw. Amosy Zephania, aliishukuru Sekta ya Mifugo (SMZ) kwa maandalizi mazuri ya kikao hicho ambacho kilitanguliwa na kikao cha siku moja cha wataalamu wa sekta hizo kutoka pande mbili za Muungano na kusisitiza umuhimu wa vikao hivyo “vikao hivi tuvipe umuhimu wa kipekee ili tuweze kufanya tahmini ya maendeleo ya sekta zetu”. Alisisitiza Kaimu Katibu Mkuu. 

Kaimu Katibu Mkuu pia aliongeza kuwa kwa kuendelea kushirikiana kupitia vikao na utekelezaji wa maazimio yanayoridhiwa na pande zote mbili, sekta za Mifugo zitapiga hatua na kunufaisha wananchi kiuchumi kulingana na idadi kubwa ya mifugo iliyopo nchini. 

Bw. Zephania alisisitiza kuwa ni vyema wataalam wa sekta za Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kiutendaji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu ili kupunguza au kuondoa kabisa kero na changamoto zinazowakabili wafugaji wa Tanzania. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Maryam Juma Sadallah akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo (SMT) Bw. Amosy Zephania, alishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) kwa kuendelea kushirikiana nao ikiwa ni pamoja na kutimiza makubaliano ya kukutana kwenye vikao kazi kama walivyokubaliana. 

Aidha Bi. Maryam aliipongeza timu ya wataalamu wa Sekta za Mifugo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa utekelezaji wa kiwango cha hali ya juu wa maazimio ya kikao kilichofanyika Juni 4, 2021 kwenye ukumbi wa TVLA jijini Dar Es Salaam, “ Nawapongezeni wataalamu wetu kwa kazi nzuri mliyoifanya ingawa sio kwa asilimia mia moja lakini mmejitahidi sana”. Alisema Bi. Maryam. 

Aidha aliwataka wataalamu kushirikishana kwenye mipango kazi yao ili iwe rahisi kusaidiana pia kutumia fursa zinazopatikana kwa faida ya pande mbili za Muungano akitolea mfano wa baadhi ya miradi ya miundombinu ya mifugo inayotarajiwa kujengwa Zanzibar kwa mkopo wa dola mil. 60 kutoka nchi ya Hungary. 

Naye Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Pemba, Bw. Hakim Vuai Shein amepongeza timu ya wataalamu kwa utekelezaji wa maazimio mbalimbali na kusisitiza kuwa matarajio ya wadau wa sekta ni kuona changamoto zao zinafikia mwisho. Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao hicho cha ushirikiano wa Sekta za Mifugo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni pamoja na kuwepo kwa makubaliano maalum kati ya Taasisi za Utafiti na Mafunzo. 

Azimio lingine ni uzalishaji wa mifugo hususan mitamba ya ng’ombe chotara ambapo SMT itatoa mbegu za mifugo dozi 1,000 kwa ajili ya kiwezesha uhimilishaji kwa wafugaji wa Zanzibar. 

Kufanya uchambuzi wa mnyororo wa gharama za uzalishaji wa mifugo na mazao yake na kuandaa maandiko ya miradi ya pamoja pia ni miongoni mwa maazimio yaliyoridhiwa na makatibu wakuu wa Sekta za Mifugo wa SMT na SMZ.

No comments :

Post a Comment