Taarifa hiyo
iliyotolewa na Gavana Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga inasema
hali hii pia ilichangia mwenendo wa riba katika soko la fedha kuendelea kuwa
tulivu na katika viwango vya chini.
“Aidha, ukuaji wa
mikopo kwa sekta binafsi umeimarika kufikia asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia
mwezi Septemba 2021, kutoka asilimia 3.2 kwa mwezi uliotangulia,” Gavana
anasema.
Anasema kamati pia,
imejiridhisha kuwa, kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa
kuendelea kuimarika kutokana na kuimarika kwa uchumi wa dunia, pamoja na hatua
za kisera zilizochukuliwa na BoT ili kuchochea upatikanaji wa mikopo kwa riba
nafuu.
“Akiba ya fedha za
kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kufikia dola za Marekani bilioni 6.7
kwa mwezi Oktoba 2021, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka
nje ya nchi kwa takriban miezi 7, sanjari na lengo la nchi na makubaliano ya
jumuiya za kikanda” Gavana anasisitiza.
Anaeleza ya kuwa kamati
imebaini kuwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imekuwa chini kidogo ya
matarajio ya awali kutokana na kuibuka upya kwa janga la UVIKO-19 katika baadhi
ya nchi, na kupanda kwa bei za nishati duniani.
“Hata hivyo, ukuaji huu
wa uchumi wa dunia unatarajia kuchangia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa
Tanzania. Kasi ya mfumuko wa bei duniani, imekuwa ikipanda, kutokana na
kuongezeka kwa mahitaji na kupanda kwa bei za nishati duniani, hata hivyo,
Benki Kuu nyingi duniani zinaona ongezeko hili kuwa ni la mpito, na hivyo
kuendelea na sera ya fedha yenye kuongeza ukwasi,” profesa Luoga anasema.
Anasema kamati inaamini
kwamba, kuongezeka kwa uzalishaji wa mafuta duniani kutapunguza kupanda kwa bei
nishati, pamoja na hayo, kamati inasisitiza umuhimu wa kuendelea kwa
upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini, na uimara wa thamani ya shillingi
dhidi ya fedha za kigeni kunakotarajia kupunguza athari ya kupanda kwa bei ya
mafuta kwenye mfumuko wa bei.
Anasema pia, Kamati
ilijadili mwenendo wa hivi karibuni wa uchumi wa ndani na kuona kuwa ukuaji wa
uchumi Tanzania Bara uliendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 4.7 katika nusu
ya kwanza ya mwaka 2021.
“Mfumuko wa bei
uliendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5, sanjari na makubaliano ya
kikanda kwa nchi za EAC na SADC. Mfumuko wa bei unatarajiwa kusalia sambamba na
lengo, licha ya kuongezeka kidogo tangu mwezi Juni 2021,” Gavana anakumbusha.
Anaeleza ya kuwa ukusanyaji
wa mapato ulikuwa wa kuridhisha, huku mapato ya kodi yakiwa zaidi ya asilimia
90 ya lengo. Wakati uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 6.5 katika robo ya
pili ya mwaka 2020 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.4 katika robo ya
pili ya mwaka 2020.
Anasema mfumuko wa bei
uliendelea kuwa chini ya lengo la asilimia 5, huku ukusanyaji wa mapato ukiwa
sawa na asilimia 73.6 ya lengo. Ambapo sekta ya nje imeendelea kuimarika
kutokana na athari za janga la UVIKO-19, ikiendelea kuwa na nakisi ndogo za
urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje kutokana na
kuanza kuingia kwa mapato yatokayo nje ya mauzo ya madini, mazao ya biashara na
shughuli za utalii.
Gavana anasema kwa
kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa hivi karibuni, pamoja na matarajio
ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo, Kamati ya Sera ya Fedha
imeridhia BoT kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwa
kipindi cha mwezi Novemba na Desemba 2021 ili kuendelea kuimarisha uchumi.
No comments :
Post a Comment