Saturday, October 30, 2021

Waziri Mkuu Awataka Mawaziri Kutotumia Wasaidizi Binafsi Katika Ofisi Za Umma






Na Ahmed Sagaff - MAELEZO

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka manaibu na mawaziri wa wizara zote nchini kuacha matumizi ya wasaidizi binafsi kwa ajili ya kuwafanyia kazi katika ofisi za umma.

Akifungua mafunzo ya viongozi hao yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi leo jijini Dodoma, Mhe. Majaliwa amesema matumizi ya walinzi na wanahabari binafsi katika ofisi za umma kunasababisha kuvuja kwa siri za Serikali.

“Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo,” ametanabahisha Waziri Mkuu.

Sambamba na hayo, Mhe. Majaliwa amewataka viongozi hao wa umma kuwa kusimamia amani na utulivu, utawala bora, kuepuka uzembe na ubadhirifu, kusimamia nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kutumia lugha ya staha.

Mengine aliyoyasisitiza ni kuunga mkono kampeni na maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa sambamba na kuzingatia itifaki na mawasiliano.

“wakati wa ziara katika Mikoa hakikisheni Wakuu wa Mikoa husika wanapata taarifa kwa wakati na ni vema kutembelea Ofisi hizo pamoja na za Chama kwa ajili ya kupata maelezo muhimu,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.

No comments :

Post a Comment