Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Bujumbura-Burundi
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 19 Octoba 2021 ametembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo Waziri Mkenda pamoja na wataalamu mbalimbali aliombatana nao amekagua kiwanda cha FOMI na kuona kinavyofanya kazi ikia ni lengo la kuona uwezekano wa kiwanda hicho kama kinaweza kuuza mbolea yake Tanzania kwa bei nafuu kwa wakulima na kupatikana kwa wingi na kwa wakati.
Prof Mkenda amesema kuwa kiwanda hicho nchini Burundi kinazalisha Tani kati ya 120,000 mpaka Tani 150,000 kwa mwaka kulingana na soko la mbolea huku kikiwa kimeanza ujenzi wa kiwanda cha kisasa Jijini Dodoma nchini Tanzania ambapo kitapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za mbolea ambazo ni zaidi ya mahitaji ya mbolea nchini Tanzania ambayo ni kati ya Tani 400,000 mpaka Tani 500,000 kwa mwaka.
Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania vilevile inaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.
Waziri Mkenda amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw Ntirampeba Simon kuwa serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega kuhakikisha kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.
“Wawekezaji wote wanaowekeza kwenye biashara ya Pembejeo Tanzania tunawahakikishia kuwa Tanzania ni nchi salama kwa uwekezaji hivyo wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwekeza” Amekaririwa Waziri Mkenda
Kwa upande wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide
Dkt Rurema amesisitiza kuwa katika muktadha wa kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya kilimo kuna mambo muhimu mawili ya kuzingatia ambayo ni maji, ardhi na mbolea na katika nchi ya Burundi sekta ya mbolea imeimarika na uzalishaji unatosheleza mahitaji ya wakulima,
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM Bw Ntirampeba Simon amesema kuwa Menejimenti ya kiwanda hicho imeendelea kufurahishwa sana kwa ushirikiano unaoonyesha wa viongozi wakuu wa Tanzania kwa kutembelea Burundi mara kwa mara hususani kukitambua na kukithamini kiwanda hicho.
Amesema kuwa mbolea inayozalishwa kiwanda hapo ni nzuri na inayohimili hali yoyote ya hewa na ardhi kwa mujibu wa utafiti walioufanya.
Awali Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ambapo amewapongeza kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya huku akiwasihi kuhakikisha kuwa wanaendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa Ubalozi unaendelea kuwa kiungo muhimu katika juhudi za serikali ya Tanzania za kuhakikisha Burundi kama nchi jirani inaendelea kuwa na Amani.
Ameongeza kuwa, ubalozi unatekeleza Diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Burundi ambazo watanzania wanaweza kunufaika nazo, kutafuta masoko ya mazao ya kilimo pamoja na bidhaa za viwandani za Tanzania, kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali baina ya Tanzania na Burundi yenye maslahi kwa nchi zote mbili.
No comments :
Post a Comment