Benki ya Equity (T) imetangaza kuongeza muda wa kutoa huduma kwa baadhi ya matawi yake ili kuitikia mwito wa wateja wake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja katika tawi la Mwenge jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Robert Kiboti amesema kuwa Benki hiyo inaendelea kuthamini uwepo wa wateja kama sehemu muhimu zaidi ya ukuaji na ustawi wake.
"Benki ya Equity inaamini kuwa huduma bora kwa wateja wetu ndio sehemu muhimu zaidi ya mafanikio. Sisi kwetu mteja ni familia. Ndio maana siku zote tumekuwa tukisisitiza kuwa kwetu wateja ni memba wetu, ni wadau wetu ni familia yetu. Tunapenda kutumia muda huu kusema asante kwa wateja wetu na kuwakumbusha ahadi zetu za kuendelea kuboresha huduma ili kufikia matarajio yao kwetu” alisema.
Kiboti aliongeza kuwa Kutokana na maombi ya muda mrefu ya wateja wa maeneo ya Mwenge na jirani, ambao wengi wa ni wafanyabiashara na wajasiriamali, Benki imeamua kuongeza muda wa kazi kwa tawi hilo.
“Kuanzia sasa na kuendelea, kila Jumamosi, tawi hili litafanya kazi kutoka saa tatu asubuhi mpaka saa kumi jioni, wakati kwa siku za Jumapili, tawi hili litafanya kazi kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa nane mchana” alisema Kiboti.
Kiboti pia alisema kuwa Benki itatumia wiki ya Huduma kwa Wateja kuhamasisha wateja kutumia njia mbadala za kupata huduma kama kupitia simu za mkononi yaani EazzyBanking, ATM, Huduma kwa njia ya mtandao yaani Eazzynet , na pia kupitia Mawakala wa Benki hiyo waliopo kila kona ya nchi.
“Katika wiki hii, mimi na timu yangu tutatembelea wateja katika maeneo yao ya biashara ili kubadilishana uzoefu na kusikiliza changamoto zao. Tunataka kuwafikia katika maeneo yao na kufanya nao mazungumzo ya ana kwa ana ili kwa pamoja tufanikiwe kufikia malengo yetu” alisema.
No comments :
Post a Comment