Wednesday, September 1, 2021

VYETI VYA KIELEKTRONIKI VYA CHANJO YA UVIKO-19 KUANZA KUTOLEWA

Na WAMJW-Dodoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuboresha suala la upatikanaji wa vyeti kwa njia ya TEHAMA kwa wanachi wenye uhitaji wa vyeti vya kielectroniki ili kuwaondolea wananchi usumbufu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurungenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Leonard Subi leo wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa watoa huduma wamewezeshwa kuhakiki na kuingiza taarifa za waliochanjwa kwenye mfumo wa kutoa vyeti vya kielectroniki kwa wananchi wote wenye uhitaji wa haraka wa vyeti hivyo katika vituo walivyopatiwa chanjo.

Dkt. Subi amesema kuwa ili kuwaondolea usumbufu wananchi waliochanjwa kabla ya mfumo ambao wanahitaji vyeti vya kielectroniki, tunashauri waende kwenye vituo walipopatia chanjo ya UVIKO-19 wakiwa na cheti cha nakala ngumu na fomu waliojaza ya uhiari (consent form) na kuwapatia watoa huduma ili kuhakiki na kuwapatia cheti cha kielektroniki.

‘Baada ya kuingizwa kwa taarifa za waliochanjwa watapokea ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu zao za mkononi ambapo ujumbe huo una “link” inayowezesha kuona na kuchapisha cheti mahali popote’. Amebainisha Dkt.Subi.

Aidha, Dkt. Subi ameongeza kuwa watoa huduma zaidi ya 1994 kutoka kwenye vituo vinavyotoa chanjo, waratibu wa chanjo wa Halmashauri na Mikoa, Waganga wakuu wa Halmashauri na Mkoa wamepatiwa mafunzo na kupewa idhini ya kuingia kwenye mfumo ili kutekeleza wajibu wao wa kuwahudumia ipasavyo wananchi kwenye maeneo yao bila usumbufu.

Wananchi wanaweza kuwasiliana kwa simu au jumbe za maandishi kupitia namba za viongozi, kwa wananchi wa Dar se salaam waliochanjwa eneo la ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere na maeneo mengine wanaombwa kufika ofisi za Mpango wa Taifa wa chanjo zilizopo Mabibo au wawasiliane na Meneja Mipango kwa namba za simu 0766-368489 au Mr. Bulula 0713-345508 au Dkt. Mwendwa 0713-256855 kwa maelezo zaidi.

Dkt. Subi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kupata chanjo ikiwa ni kinga dhidi ya UVIKO-19 kwani chanjo hizi ni salama, zina ufanisi na ubora uliothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuhakikiwa na vyombo vyetu ikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

‘Niwaombe sana wananchi tuendelee kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipakusi, kuvaa barakoa ipasavyo, kuepuka misongamano, Lishe bora na kufanya mazoezi ili kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa UVIKO-19’. Amesema Dkt. Subi.

No comments :

Post a Comment