Thursday, September 2, 2021

FURAHIKA YATANGAZA NAFASI ZA WALIMU WA KUJITOLEA, KUTOA MAFUNZO LUGHA ZA KIGENI BURE


SHIRIKA La Furahika Education Organization limetangaza nafasi za walimu wa kujitolea katika chuo cha Furahika kilichopo Buguruni Malapa mkoani Dar es Salaam ili kuweza kuwasaidia watoto wakike wanaopata mafunzo bure kutoka katika chuo hicho pamoja na kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha huduma ya elimu inamfikia kila mmoja hasa watoto wakike. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi David Msuya amesema, fursa hiyo ni kwa malengo ya kuwasaidia wanafunzi wa kike wanaopata mafunzo bure chuoni hapo pamoja na walimu hao kupata ujuzi zaidi katika fani mbalimbali walizosomea.

Amesema kuwa walimu wanaohitajika ni wanawake kutoka katika fani za biashara na manunuzi, TEHAMA, kilimo na ufugaji, usindikaji wa mazao ya kilimo hasa kahawa na pamba pamoja mbunifu wa mavazi katika kozi ushonaji na walimu wenye sifa na vigezo wamealikwa kutuma maombi kupitia barua pepe ya chuo chuoeducationmaendeleo@gmail.com. 

Aidha amesema, usahili wa wanafunzi unaendelea na wanaendelea kupokea wanafunzi kutoka mikoa ya Arusha, Iringa, Manyara na Mtwara na maombi yatumwe kupitia website ya chuo na kueleza kuwa kwa waombaji wa kozi ya ualimu ngazi ya cheti wanatakiwa kuwa na D tano na watapata ujuzi wa kufundisha na michezo ya watoto mashuleni na saikolojia.

Vievile Msuya amesema kuwa chuo hicho kimetoa fursa kwa walimu kusoma kozi za lugha za kigeni ikiwemo Kichina, Kifaransa na Kiitaliano kwa malengo ya kuongeza maarifa, kukuza ufanisi na kupata uwezo wa kuwasiliana na wageni katika kukuza maarifa na kutangaza vivutio vya utalii na mafunzo hayo yatatolewa bure mara baada ya kazi kuanzia septemba 20 mwaka huu huku mkoa wa Pwani ukitarajiwa kuwa wa kwanza kwa walimu kupatiwa mafunzo hayo.

Chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali bure kwa watoto wakike ili kuwawezesha kujikwamua kifikra na kiuchumi na kozi zinazotokewa ni pamoja na kozi ya kompyuta ngazi ya cheti, ukalimani wa lugha alama, ushonaji, mapishi, muziki na mafunzo ya hoteli na kuanzia Oktoba Mosi kitaanza kutoa mafunzo wanaorudia mitihani ya kidato cha nne na sita.

No comments :

Post a Comment