Friday, September 3, 2021

CHAMURIHO AWATAKA WAHANDISI VIJANA KUJENGEWA UWEZO

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akihutubia wahandisi katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Malongo, akisisitiza jambo kwa wahandisi (hawap pichani), katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Prof. Ninatubu Lema, akizungumza na wahandisi (hawapo pichani), katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

Wahandisi 632 wakila kiapo cha utii katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akimkabidhi leseni ya uhandisi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Eng. Robert Gabriel, mara baada ya kula kiapo cha utii katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) katika maadhimisho ya 18 ya Siku ya Wahandisi, jijini Dodoma.

PICHA NA WUU

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amezitaka Taasisi zote zinazohusika na kazi za kihandisi nchini kuweka kipengele cha kuwajengea uwezo wahandisi vijana katika mikataba yote ya ujenzi itakayoingiwa na Serikali kuanzia sasa.


Akifungua mkutano wa 18 wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), jijini Dodoma, Waziri Chamuriho amesema sera na muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha wahandisi hususani vijana kuwa na uwezo wa kutosha kusimamia miradi ya ujenzi inayoendelea nchini na inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Hakikisheni miradi mikubwa kama ya SGR, Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, miradi ya maji, bomba la mafuta, madaraja makubwa, ujenzi wa meli na barabara unahusisha moja kwa moja wahandisi vijana”, amesema Waziri Chamuriho.

Amebainisha kuwa Serikali imejipanga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi yake ya maendeleo hivyo ni wajibu wa sekta binafsi na serikali kushirikiana kuwawezesha wahandisi kupata uzoefu utakaowasaidia kufanya kazi ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Chamuriho, amewashukuru Benki ya Dunia na Serikali ya Norway kwa kufadhili programu mbalimbali za kuwajengea uwezo wahandisi hususani wanawake na kutoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Malongo, ameitaka ERB kufanya tathimini ya maazimio yaliyofikiwa mwaka jana kuona kama yametekelezwa na hivyo kujipima katika yale matarajio yaliyofikiwa.

Amezungumzia umuhimu wa kufuatilia wahandisi wahitimu wanaofanya vizuri katika masomo yao ili kuona kama wanafanya vizuri katika utendaji wa kazi zao kama ambavyo maadili ya taaluma yao yanavyowataka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Prof. Ninatubu Lema, zaidi ya wahandisi 32,145 wamesajiliwa na bodi hiyo tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo.

Akiwakaribisha wahandisi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amewataka wahandisi kuwekeza katika mkoa huo ili kuufanya mji mkuu wa nchi kuwa katika viwango bora vya miundombinu.

Zaidi ya wahandisi 600 wamekula kiapo cha utii leo katika kikao hicho na kukabidhiwa leseni tayari kwa kuanza kazi za kihandisi. 

No comments :

Post a Comment