Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Wateja wa benki ya Exim Bi. Agnes Kaganda (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma mpya ya bima ya benki hiyo ijulikanayo kama "Bima Tu, Malipo Tuachie” wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha huduma za Bima kwa mabenki wa benki hiyo Bw Melchizedeck Muro (wa pili kushoto) pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.
Katika juhudi za kuboresha zaidi huduma zake sambamba na kuongeza ujumuishaji wa jamii zaidi katika sekta ya kifedha nchini, Benki ya Exim Tanzania leo imezindua huduma mpya ya bima ijulikanayo kama "Bima Tu, Malipo Tuachie”.
Katika kufanikisha mpango huo, benki hiyo imeshirikiana na kampuni kubwa za bima nchini ili kuwaletea wateja wake huduma bora za Bima zikiwemo, Bima ya Afya, Bima ya safari na Bima ya Maisha ambazo zote zitatolewa pamoja chini ya benki hiyo.
Huduma hiyo itatolewa kupitia matawi yote ya benki hiyo nchini kwa kushirikiana na makampuni 10 ya bima kama ilivyoidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA).
"Kampuni hizo za bima ni pamoja na Jubilee Insurance, Fist Assurance, Heritage Insurance, GA Insurance, Alliance Life Assurance, Britam Insurance, UAP Insurance, ICEA Lion General Insurance, Strategies Insurance, na Alliance Insurance corporation.” Alitaja Bi. Agnes Kaganda, Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Wateja wa benki ya Exim wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
"Lengo letu ni kuondoa usumbufu kwa wateja kwa kuongeza thamani kwenye huduma za bima ikiwemo pamoja na urahisi wa kuripoti madai, mashauriano, ufuatiliaji na usuluhishi, mchakato rahisi wa madai, kupunguza athari ya jumla ya gharama kwa kusimamia vyema hatari zinazoweza kujitokeza, urahisi katika kusajili bima mpya ambapo wateja watapewa taarifa za kuisha kwa kipindi cha bima zao kidigitali sambamba na kupatiwa msaada wa karibu katika kusajili bima upya.’’
"Zaidi, Benki ya Exim inatambua kuwa wateja huwa wanahitaji suluhisho kamili la kifedha na ushauri kulingana na mahitaji yao maalum na hali zao za sasa na sio bima ya jumla. Wateja wanataka suluhisho na sio huduma tu na hili tumelizingatia katika huduma hizi.’’ Alisema.
Kwa upande wake Bw Melchizedeck Muro ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Bancassurance cha benki hiyo alitaja faida zingine za huduma hiyo kuwa ni pamoja na huduma ya huduma zote katika sehemu moja (One Stop Shop) ambapo benki, kama msambazaji wa huduma hizo, itawawezesha wateja wake kupata huduma za bima pamoja na huduma nyingine za kifedha kama vile kupata mkopo kwa ajili ya malipo ya tozo za bima (Insurance Premium Financing) zote kutoka sehemu moja na katika kiwango cha ushindani.
"Kwa muda mrefu huduma za Bima zilikuwa na sintofahamu kwenye baadhi ya masuala lakini kupitia mpango huu changamoto hii inakwisha kwasababu kila kitu kinakuwa cha uhakika,’’
‘’Wateja wanahitaji ufanisi katika dhana ya kitaalam na imani wanapohitaji huduma za kibima kwa kuwa wanahitaji kupata ushauri kabla ya wao kusajili bima zao. Benki ya Exim imejipanga kwenye hilo na tutaweza kuwashawishi katika hilo. Hii inaenda sambamba na utaalam tulionao katika kubuni huduma hizi za bima na pia utoaji wa mapendekezo bora.” Aliongezea
Kwa mujibu wa Ndugu Muro huduma hizo za Bima zinapatikana na kutolewa kwa wateja wa sasa wa benki hiyo pamoja na umma kwa ujumla.
No comments :
Post a Comment