Thursday, August 12, 2021

WASIMAMIZI WA SEKTA YA FEDHA BARANI AFRIKA WATOA KIPAUMBELE KWA MAKUNDI YALIYO KATIKA HATARI KUBWA YA KUTENGWA NA HUDUMA ZA FEDHA

********************************

Wanawake, vijana, wajasiriamali na kampuni ndogo na za kati (MSMEs) barani Afrika wako katika hatari kubwa ya kutengwa na huduma za fedha katika kipindi cha UVIKO19, imesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Taasisi ya Kimataifa ya Huduma

Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion-AFI) 

DODOMA / KUALA LUMPUR (12 Agosti 2021) – Benki Kuu ya Tanzania na AFI, taasisi inayoongoza duniani kwenye sera na kanuni za huduma jumuishi za fedha, kwa pamoja

zimefanya mkutano tarehe 12 Agosti kwa ajili ya viongozi wa taasisi za usimamizi wa sekta ya fedha barani Afrika kutafuta utatuzi kwa makundi yaliyo kwenye hatari ya kutengwa kutokana na janga la UVIKO-19.

Katika kauli mbiu  “Ubunifu katika mikakati ya usimamizi wa sekta ya fedha ili kukwamua wanawake, vijana, wajasiriamali na kampuni ndogo na za kati katika hatari ya kutengwa kutokana na janga la UVIKO-19 barani Afrika”,benki kuu na muungano wa uongozi wa sera za huduma jumuishi za fedha duniani wamekutana kimtandao kama sehemu ya mkakati wake katika nchi za Afrika. Ambapo, viongozi wanaounda Mkakati wa Kisera wa Huduma Jumuishi za Fedha barani Afrika (AfPI) wamejadili, nakubadilishana uzoefu na kutafuta suluhu za kibunifu ili kukwamua makundi yaliyo katika hatari ya kutengwa.

“Utendajikazi wetu wa muda mrefu pamoja na AFI umejengwa katika pande mbili, ambazo ni ushirikiano wa kisera na usaidizi wa kitaalamu katika kuhakikisha hatuyaachi nyuma makundi ambayo yanaathirika zaidi katika majanga, mfano katika janga la UVIKO-19,” alisema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga. 

“Hivyo, tunafurahi kufanya kazi pamoja na AFI kwa miaka miwili mfululizo katika kuhakikisha wajumbe wa AfPI tunakutana, na kushiriki kwa kutoa uzoefu wetu na kujifunza toka kwa wenzetu,” alisema Gavana Prof. Luoga.

Benki Kuu ya Tanzania imewekuwa mstari wa mbele katika harakati za huduma jumuishi za fedha barani Afrika kwakuwa mfano katika kudhibiti mtikisiko wa kifedha kwa vikundi ambavyo vipo katika hatari za kutengwa na huduma za fedha ili kufufua uchumi. Baadhi za hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kulegeza sera za fedha na kuzihamasisha benki kuahirisha ulipaji wa mikopo, kupunguza riba na kuongeza muda kulipa mikopo ili kutoa unafuu wa kifedha kwa wateja. Aidha, benki kuu imekuwa mstari wa mbele katika jitihada za Tanzania katika kukuza mifumo ya malipo kidigitali kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa muingiliano (interoperability) katika malipo na kuanzishwa kwa mfumo wa kusajili watoa huduma za fedha. 

Katika kikao hicho, Gavana Profesa Luoga ameungana na magavana na manaibu gavana wenzake wa benki kuu za Burundi, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Namibia, Rwanda, Senegal, Seychelles, Sierra Leone na Zimbabwe. Ushiriki huu mkubwa wa viongozi wa AfPI umethibitisha umuhimu wa benki kuu katika kufanikisha ufufuaji wa chumi za nchi zao.

“Wanachama wa AFI barani Afrika wamechangia katika kuongezeka kwa matumizi ya huduma za fedha kidigitali (DFS) na teknolojia zingine bunifu kama matokeo ya sera za kupambana na janga la UVIKO-19 ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana hapo awali katika huduma jumuishi za fedha hayapotei ikiwa ni pamoja na kuwainua wale ambao wapo chini kiuchumi,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa AFI, Dk. Alfred Hannig .

Licha ya kwamba kazi hii siyo rahisi, Dk. Hannig alieleza matumaini yake kwa wanachama wa AfPI kuendelea kutoa miongozo bora ya kisera na kukuza mtandao ili kuweza kuyafikia malengo yao.

“Kwa takribani muongo mmoja sasa, hasa miaka miwili iliyopita tangu janga la UVIKO-19 kutokea, AfPI imeweka msingi imara kwa ajili ya ushirikiano, kujitathmini kimafunzo na kubadilishana ujuzi baina ya taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha, washiriki wa masoko na wadau wengine barani Afrika,” Dk. Hannig alisisitiza. 

AfPI, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Mkakati wa Kisera  kwa Afrika kutumia Huduma za Fedha kupitia Simu za mkononi (African Mobile Financial Services Policy Initiative), ilianzishwa mwaka 2012.

Kabla ya kuanza kukutana pamoja chini ya AfPI, mikutano iliyokuwa ikifanyika ilikuwa  ni pamoja na vikao vya Kundi la Wataalam wa Huduma Jumuishi za Fedha (EGFI), mafunzo kwa wanachama na mijadala yapamoja na taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha na wadau wa sekta binafsi kutoka nchi zilizoendelea. 

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Afrika inaendelea kuathiriwa na janga la UVIKO-19 kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu lilipoanza. Athari hizo ni pamoja na kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, kupungua kwa mauzo na kufungwa kwa biashara ambapo zote kwa pamoja zinaathiri makundi maalumu katika jamii ikiwa pamaoja na wanawake, vijana na wajasiriamali na  kampuni ndogo na za kati (MSMEs).

Kumekuwa na hasara kubwa kimapato na kuyumba kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake kutokana na sehemu kubwa ya shughuli hizo kutokuwa rasmi na kutegemea sekta nyingine kama utalii, ambayo imeathirika pakubwa na janga la UVIKO-19. Aidha, wanawake wamejikuta katika majukumu makubwa Zaidi majumbani kwakufungwa kwa shule, hali ambayo imepunguza uwezo wao wa kujishughulisha kiuchumi.

Vijana barani Afrika wataona athari za janga hili si muda mrefu sana toka sasa. Hivi sasa, vijana wengi hawana ajira na wengine wamejiajiri katika sekta zisizo rasmi ambazo zimeathirika vibaya na UVIKO-19. Vijana pia, hawana vitu vya kuweka dhamana kama wanataka kupata mikopo kutoka taasisi rasmi za fedha.

AfPI ni jukwaa la msingi na la kwanza kwa wanachama wa AFI barani Afrika katika kusaidia na kuandaa sera za huduma jumuishi za fedha na mipango ya udhibiti na usimamizi, na kuratibu jitihada za kikanda za kubadilishana uzoefu. AfPI yenye wanachama hai 39, ndiyo mkakati mkubwa zaidi wa kikanda wa AFI ambao una wanachama hai wengi wakiwa na machapisho mengi yenye tija yaliyochapishwa ndani ya kipindi cha miezi 12 tu iliyopita, ikiwa ni pamoja na mipango ya sera ya kikanda inayolenga kuimarisha mtandao wa mawakala wa huduma za fedha za kidigitali (DFS) na kuimarisha mazingira ya kuziwezesha kifedha biashara ndogo ndogo barani Afrika.

Kutoka katika ofisi ya kanda ya AFI jijini Abidjan, Côte d’Ivoire, AfPI imewaleta pamoja watunga sera na taasisi za udhibiti na usimamizi na wadau wengine wanaohusika katika kuwezesha utekelezaji wa sera zenye kuchochea ubunifu katika huduma jumuishi za fedha barani Afrika. 

Mkutano wa viongozi ni sehemu ya mikutano ya siku nne ya wanachama wa AfPI. Kabla ya mkutano huu wa ngazi ya juu kabisa, wadau mbalimbali wa huduma jumushi za fedha walikutana kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 9-11 Agosti kujadili masuala muhimu yanayohusu udhibiti/usimamizi na masoko. Pia walikuwepo wawakilishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Benki ya Ulaya (European Banking Authority), mtandao wa malipo ya fedha kati ya nchi na nchi (Cross-border payments network Thunes), kampuni ya huduma za kifedha ya Visa na kampuni ya simu ya Vodacom kutoka Afrika Kusini.  

Wadau wa sekta ya umma na binafsi walikutana kujadili kuhusu huduma za fedha kwa makundi yaliyo katika hatari, wakati huohuo wadhibiti/wasimamizi kutoka nchi zinazoendelea na zilizoendelea walibadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuwezesha ubunifu wa kiteknolojia katika masuala ya fedha. Aidha, wanachama wa AfPI walipata mafunzo kuhusu miundombinu ya malipo ya kidigitali, huduma na matumizi ya malipo ya bila kutumia nywila (contactless payment).

Kupitia matukio ya AfPI na AFI, wadhibiti/wasimamizi wa sekta ya fedha wanatoa mchango mkubwa katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN Sustainable Development Goals) kwakufanya mijadala inayolenga maendeleo endelevu, wataalamu wao kuandaa na kutumia misingi ya kijamii ya uwajibikaji katika fedha ili kuuweka uchumi katika mkondo wa ukuaji endelevu, ambao ni muhimu kwa ustawi wa vizazi vijavyo.

Tukio hili, kwa sehemu linagharamiwa na Mfuko wa Wahisani wa AFI kwa ajili ya utekelezaji wa Sera za Huduma Jumuishi za Fedha (AFI’s Multi-Donor Financial Inclusion Policy Implementation Facility), pamoja na ushiriki wa Taasisi ya Maendeleo ya Ufaransa (French Development Agency), Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani(the German Federal Ministry for Economic Cooperation and Development) na Wizara ya Fedha ya Lasembagi (Ministry of Finance of the Grand Duchy of  Luxembourg).

 

Kwa maelezo zaidi au kuomba mahojiano, tafadhali wasiliana na:

Dodoma: Zalia Mbeo kupitia barua pepe zambeo@bot.go.tz  au simu namba + 255 787 708 600 au +255 767 708 600 na +255 26 296 2586

Luxembourg: Monika Lajhner kupitia barua pepe monika.lajhner@afi-global.org au simu namba +352-45-68-68-700.

 

Kuhusu Benki Kuu ya Tanzania 

Makao Makuu yake ni Dodoma, Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha nchini. Pia, ina wajibu wa kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kuendeleza utulivu, usalama na uthabiti wa mfumo wa fedha nchini na kupunguza vihatarishi vya hasara kwa wenye amana. Benki Kuu ilijiunga na mtandao wa taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta za fedha duniani chini ya AFI mnamo Februari 2010. Tangu wakati huo imetayarisha na kutekeleza sera na maboresho ya udhibiti na usimamizi 12 ili kukuza huduma jumuishi za fedha. Pia imefanikiwa kutekeleza shabaha 5 kati ya 13 za Azimio la Maya, ikiwemo shabaha ya kukuza na kuendeleza huduma za uwakala wa mabenki.

https://www.bot.go.tz/

Kuhusu AFI

AFI ni taasisi inayoongoza duniani kwenye sera na kanuni za huduma jumuishi za fedha. Hadi hivi sasa, AFI ina zaidi ya taasisi wanachama 100 ambazo zinaunda mtandao wa AFI unaojumuisha benki kuu, wizara za fedha na taasisi zingine za udhibiti/usimamizi na utungaji sera za fedha kutoka nchi 89 zinazoendelea na masoko yanayoibukia. AFI inawawezesha watunga sera kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma bora za fedha kwa watu ambao hawazipati kwa njia ya sera endelevu na shirikishi na matumizi yenye ufanisi ya teknolojia ya kidigitali. www.afi-global.org 

 

Kuhusu hatua za Kisera za AFI kupambana na janga la UVIKO-19 (AFI COVID-19 Response) Hatua za Kisera za AFI kupambana na janga la UVIKO-19 zinalenga kuchukua hatua za uratibu wa kisera ili kusaidia wanachama wake kukabili madhara yatokanayo na athari ya janga la UVIKO-19 hasa katika utekelezaji wa sera ya huduma jumuishi za fedha, kwa wajasiriamali na kampuni ndogo ndogo (MSMEs) pamoja na makundi ya kijamii yaliyo katika hatari ya kutengwa na huduma za fedha. Hatua inazochukua AFI ni pamoja na zile za haraka, zinazotokana na mahitaji, na kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha hatua za haraka za kisera na kiudhibiti zinachukuliwa katika nchi zilizoathirika sana. Hatua za Kisera za AFI zimeandaliwa ili kutimiza mahitaji ya muda mfupi na muda wa kati, https://www.afi-global.org/covid-19/ 

 

No comments :

Post a Comment