Thursday, August 12, 2021

TIC YAFANYA UTAFITI NA KUIBUA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MRADI WA RELI YA KISASA YA SGR

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekzaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kituo hicho leo Jijini Dar es salaam.

***************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM  

Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kwa kushirikiana na Wadau wengine Serikalini kimefanya

utafiti ili kuibua fursa za uwekezaji zilizo usholoba wa Reli ya Kisasa ya SGR kwa kuanza na eneo kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Ameyasema hayo leo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi alipokaa kikao na waandishi wa habari leo katika ofisi za TIC Jijini Dar es Saalaam.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Kazi amesema wadau walishiriki katika utafiti huo ni pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Fedha na Mipango, Shirika la Umeme (TANESCO), na TPDC. Utafiti huu umeibua fursa au miradi thelathini (30) ya uwekezaji.

Amesema kati ya miradi hiyo 30, miradi mitano (5) ni miradi ya miundombinu wezeshi (Enabler Projects) ambayo utekelezaji wake unategemea bajeti ya Serikali na miradi 25 ni fursa za uwekezaji ambazo zinategemea zaidi uwekezaji kutoka kwenye sekta binafsi

“Baada ya utafiti huu wa awali, TIC iliwasiliana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) nchini ili kushirikiana na kuandaa maandiko ya awali ya miradi (Project concept notes) ambapo tayari Concept notes za miradi 19 imeandaliwa. Kati ya miradi hiyo 19, miradi tisa (9) imekidhi sifa za kufanyiwa upembuzi yakinifu wa awali (prefeasibility studies) kabla ya kufanya upembuzi yakinifu (Feasibility studies) wakati miradi 10 inaendelea kuboreshwa ili kukidhi vigezo”. Amesema Dkt.Kazi.

Aidha amesema kituo hicho kimeendelea kuhamisisha uwekezaji wa Sekta binafsi nchini sambamba na uwekezaji kutoka nje ya nchi. Katika kutekeleja hilo, jitihada zimefanyika kutafuta ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo inatoa mikopo nafuu ili kuwezesha uwekezaji.

Sambamba na hayo amesema katika mwaka wa fedha 2020/21, TIC imehamasisha sekta binafsi kutumia fursa ya mikopo nafuu kutoka AfDB ambapo zaidi ya kimiradi 100 iliwasilishwa TIC.

“Katika kuchambua miradi hiyo, miradi 54 ilikidhi vigezo na kuwasilishwa AfDB na miradi minne kati ya hiyo imefudhu katika hatua za awali za AfDB”. Amesema

 

No comments :

Post a Comment