Monday, August 23, 2021

TCU YAFUNGUA DIRISHA LA PILI LA UDAHILI WA SHAHADA YA KWANZA 2021/2021

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, (TCU) Profesa Charles Kihampa akizungumza na waandishi wahabari kuhusu kukamilika kwa dirisha la kwanza na kufunguliwa kwa dirisha la pili la udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2021/2022 leo Augusti 23,2021 jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, (TCU) Profesa Charles Kihampa akizungumza na waandishi wahabari kuhusu kukamilika kwa dirisha la kwanza na kufunguliwa kwa dirisha la pili la udahili la shahada ya kwanza mwa mwaka wa masomo 2021/2022 leo Augusti 23,2021 jijini Dar es Salaam kululia kwake ni Mkurugenzi wa uratibu wa Udahili na utunzaji wa Kanzidata wa Tume hiyo Dkt Kokuberwa Kulunzi-mollel

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufungua kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2021/20212 utakaokuwa kwa siku sita kuanzia kesho Augusti 24 hadi Septemba 6, mwaka huu.

Pia tume imewasisitiza waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili ama kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbali mbali kutumia fursa hiyo kwa kutuma maombi yao ya udahili kwa vyuo wanavyovipenda.

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof.Charles Kihampa amesema hayo leo Agosti 23,2021, alipokuwa akitangaza kukamilika kwa udahili wa awamu ya kwanza na kufunguliwa kwa awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza 2021/2022.

Kufuatia kufunguliwa kwa awamu ya pili, tume pia imezielekeza Taasisi za Elimu ya Juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi huku waombaji wa vyuo pia wakihimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili.

“Waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenyen kalenda ya udahili iliyotolewa na TCU kama inavyooneshwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz)”. Amesema Prof.Kihampa.

Aidha Prof.Kihampa amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 92,809 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 74 vilivyoidhinishwa kudahili huku programu 724 zikiwa zimeruhusiwa kudahili ukilinganisha na programu 686 mwaka 2020/2021 na kwamba mwaka huu kuna jumla ya nafasi 164,901 ikilinganishwa na nafasi 157,770 kwa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la nafasi 7,131 za shahada ya kwanza sawa na asilimia 4.5.

"Katika awamu hii ya kwanza ya udahili jumla ya  waombaji 68,019 sawa na asilimia 73.2 wamepata udahili vyuoni, mwenendo huu wa udahili wa Awamu ya kwanza kwa kipindi cha miaka minne (2018/2019 hadi 2021/2022 ) unaoonyesha ongezeko kubwa la waombaji ni kiashiria cha ongezeko la wahitimu kidato cha sita na wale wa stashahada", amesema Prof.Kihampa.

Aidha Tume imewataka waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao kwa kuchagua chuo kimojawapo kuanzia kesho Augusti 24, 2021 hadi Septemba 6 2021 kwa kutumia namba zao za simu ama barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

Pia TCU imewaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.

No comments :

Post a Comment