Thursday, August 19, 2021

TANZANIA YASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA MNYORORO WA UONGEZAJI WA THAMANI.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa India Mhe.Binaya Srikanta Pradhan. Balozi Mteule Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amekabidhi nakala za hati hizo katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Uholanzi Mhe. Weibe Jacob DE BOER. Balozi Mteule Mhe.Weibe Jacob DE BOER  amekabidhi nakala za hati hizo katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dar es Salaam. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Misri hapa Nchini Mhe.Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa. Katika mazungumzo yao Viongozi hao wametia msisitizo kuhusu uwekezaji katika mnyororo wa uongezaji wa thamani wa madini,vito vya thamani,uvuvi katika eneo la bahari la kina kirefu(deep sea fishing) afya,miundombinu pamoja na mifugo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini hapa Nchini Mhe.CHO tae –ick na kuzungumzia maeneo ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha diplomasia,uwekezaji na biashara. 

………………………………………………………………………….

Tanzania na India zimekubaliana kuweka msisitizo katika uwekezaji katika

mnyororo wa uongezaji wa thamani wa madini,vito vya thamani pamoja na mazao mbalimbali ikiwemo korosho ili kuuza bidhaa badala ya kuendelea na utamaduni wa kusafirisha malighafi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa msisitizo huo wakati akipokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa India hapa nchini Mhe. Binaya Srikanta Pradhan na kuongeza kuwa njia pekee kwa Tanzania kuongeza ajira na kupunguza umasikini ni kuwekeza katika mnyororo wa uongezaji wa thamani katika bidhaa za kilimo pamoja na madini.

Pia Balozi Mulamula amepokea nakala za hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Weibe Jacob DE BOER ambaye ameeleza kufurahishwa na mahusiano ya kihistoria yaliyopo baina ya Nchi hizo mbili.

Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Misri hapa Nchini Mhe Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa ambapo viongozi hao wamezungumzia juu ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi hususani uvuvi katika eneo la bahari lenye kina kirefu (deep sea fishing),viwanda vya nyama lakini pia katika sekta ya afya kwa kujenga hopitali kubwa Jijini Dodoma.

Pia Balozi Mulamula kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini hapa Nchini Mhe. CHO tae –ick na kuzungumzia maeneo ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha diplomasia,uwekezaji na biashara. 

No comments :

Post a Comment