Thursday, August 12, 2021

SERIKALI YA ZANZIBAR YAELEKEZA NGUVU KATIKA KUIRUDISHA HADHI NA THAMANI YA KARAFUU YAKE

*******************************

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo pamoja na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kujikita katika kufuatilia uzalishaji wa karafuu ili kukuza hadhi ya Zanzibar katika uzalishaji na kuinua soko lake duniani.

Akizungumza katika kikao na wadau pamoja na wakulima wa zao la karafuu (Agost 12), chenye lengo la kuelezea ‘Muelekeo Mpya Wa Serikali katika kuboresha biashara ya karafuu huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Othman amesema kukosekana kwa utaratibu huo kwa muda mrefu “ndio chanzo cha kukosa karafuu zenye kiwango, uzalishaji mdogo pamoja na kupoteza soko lake duniani.”

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais ameitaka Wizara na shirika hilo kuwekeza nguvu zake katika eneo hilo kupitia wataalamu watakaotoa Elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kuzalisha karafuu  kwa lengo la kupata karafuu zenye kiwango bora.

“Zanzibar ndio sehemu pekee iliyokuwa ikitoa karafuu nyingi na zenye ubora katika soko la dunia takriban asilimia 90, lakini kiwango chetu kwa sasa kipo chini sana.Nijukumu letu kupambana ili kuirudishia hadhi yake karafuu ya Zanzibar na kuinua kipato cha mkulima wa zao hilo” alisisitiza Makamu huyo wa Kwanza.

Akizungumzia juu ya mashamba ya Eka, Mhe. Othman amewataka watendaji wa wizara hiyo kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali katika ufuatiliaji wa mashamba hayo kwa lengo la kuondosha matatizo yanayoibuka na kupoteza nguvu za wakulima hao.

Kwa upande mwengine, amelitaka Shirika la ZSTC kufanya kazi katika utaratibu utakaowapa wepesi wakulima hao, ikiwemo kutoa utaratibu na muongozo juu ya upatikanaji wa malipo yao kwa lengo la kuondosha matatizo yanayojitokeza.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan, amesema wizara yake ina mpango kwa kufanya utafiti juu ya miche ya mikarafuu inayotolewa na serikali kwa lengo kuondosha tatizo lililopo la kutokudumu kwa miche hiyo jambo linalorudisha nyuma juhudi za wakulima katika shughuli zao.

Nao wadau mbali mbali wa karafuu wameiomba serikali kuondoshwa kwa wanunuzi wa karafuu mbichi pamoja na kupewa taaluma ya mambo yatakayoongeza ubora katika kufanya shughuli zao za kilimo.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, viongozi mbali mbali wamehudhuria wakiwemo wakuu wa Mikoa, wakuu wa vyombo vya Ulinzi na usalama,  watendaji mbali mbali wa serikali  pamoja na wadau wa zao la Karafuu.

Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar

 

No comments :

Post a Comment