Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam leo Agost 03,2021 akitokea Nchini Rwanda baada ya kukamilisha ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe
03 Agosti, 2021 amehitimisha Ziara yake ya siku mbili nchini Rwanda kwa
kutembelea viwanda vitatu na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji
zinazofanywa na viwanda hivyo.
Katika kiwanda cha kwanza cha
Inyange kinachotengeneza vinywaji, Mhe. Rais Samia akiwa na mwenyeji
wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wamejionea shughuli za uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji ya kunywa, maziwa na juisi.
Aidha, Mhe. Rais Samia pia ametembelea kiwanda cha kutengeneza
simu za mkononi cha Mara Phone na kujionea hatua mbalimbali za
utengenezaji wa simu kuanzia hatua ya awali hadi kukamilika kwake.
Pia Mhe. Rais Samia ametembelea kiwanda cha uunganishaji magari cha
Volkswagen kilichopo nchini humo na kujionea hatua mbalimbali za
kuunganisha magari hayo ambayo huuzwa nchini humo.
Mhe. Rais
Samia amewaagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo na
Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe kukutana na wamiliki wa viwanda
hivyo ili kutumia fursa zilizopo katika viwanda hivyo ikiwa ni pamoja
na kuwauzia malighafi zinazopatikana nchini Tanzania.
Mhe. Rais
Samia ameagana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame katika uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Kigali na kurejea Jijini Dar es Salaam baada ya
kumaliza Ziara Rasmi ya siku mbili nchini humo.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
No comments :
Post a Comment