ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusibilo Mwakabibi na Mwenzake Eduward haule wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na matumizi mabaya ya utumishi.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Ester Martin aliyekuwa akisaidiana na wakili wa serikali Mwandamizi Mkunde Mshanga mbele Ya hakimu mkazi mwandamizi Evodia Kyaruzi imedai washtakiwa wametenda kosa hilo kati ya Machi 2020 na Machi 2021 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika shtaka la matumizi mabaya ya madaraka imedaiwa, katika kipindi hicho, mshtakiwa Mwakabibi akiwa ameajiriwa Kama Mkurugenzi na Mratibu wa mradi wa DMDP walitekeleza ujenzi wa kituo cha basi cha Buza katika Kiwanja Kilichopo buza kinachomilikiwa na Kanisa la Anglikana bila ruhusa.
Katika shtaka la Matumizi mabaya ya ofisi inadaiwa washtakiwa hao wakiwa waajiriwa wa Manispaa Ya Temeke Kama Mkurugenzi na Mratibu wa Mradi wa DMDP kwa maksudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kwenda kinyume na sheria ya Ardhi.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu kwa kuwa shtaka linalowakabili ni la uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na upande wa utetezi umeiomba mahakama itumie kifungu cha 29 (4) cha sheria ya Uhujumu Uchumi Ili kuwapa dhamana washtakiwa kwa kuwa mashtaka waliyosomewa hayajataja Kiwango cha chochote cha fedha.
Pia wameiomba Mahakama kuweka masharti nafuu ya dhamana yatakayowasiadia washtakiwa kufika mahakamani kila terehe itakayopangwa.
Hata hivyo, upande wa mashataka umedai kuwa hauna pingamizi ya dhamana
Akisoma masharti ya dhamana washtakiwa wametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. milioni Kumi ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha pesa. Pia washtakiwa wametakiwa kutotoka nje ya nchi bila Kibali.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 2, 2021 ambapo Itakuja kwa ajili ya kutajwa.
No comments :
Post a Comment