Wednesday, August 18, 2021

MRADI WA MAJI PUGU-GONGO LA MBOTO UMEONDOA CHANGAMOTO PEMBEZONI MWA JIJI



Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ritamaty Lwabulinda  akisoma taarifa ya Mradi wa Pugu - Gongo La Mboto wenye thamani ya Bilion 7.3 uliokamilika kwa asilimia 100 na wananchi 450,000 watanufaika na mradi huo kuanzia Pugu hadi Kinyerezi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambashi akipata maelezo ya mradi wa Pugu - Gongo la Mboto wenye thamani ya Bilion 7.3 kutoka kwa Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Ramadhan Mtindasi walipotembelea mradi huo uliokamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Ramadhan Mtindasi akifafanua jambo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambashi alipotembelea mradi wa Pugu - Gongo la Mboto uliokamilika kwa asilimia 100. Luteni Mwambashi ameridhishwa na mradi huo na kuwataka wananchi waendelee kulinda na kutunza miundo mbinu na vyanzo vya maji.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2021 Luteni Josephine Mwambashi akizungumza na wananchi wakati wa Kutembelea Mradi wa Pugu- Gongo la Mboto na kuwataka wananchi walinde vyanzo vya maji na miundo mbinu ya maji.



Na Zainab Nyamka,Michuzi TV

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambashi amesema uwepo wa mradi wa maji wa Pugu-Gongo la Mboto umeenda kuondoa changamoto ya maji pembezoni mwa mji.

Mradi wa Pugu-Gongo la Mboto umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wenye thamani ya Bilioni 7.3 kwa kutumia fedha za ndani.

Akikagua na  kutembelea mradi huo, Luteni Mwambashi amesema kukamilika na kuanza kwa mradi huo ni muendelezo wa huduma ya maji kuwafikia wananchi wote.

Luteni Mwambashi ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuendelea kuboresha sekta ya maji nchini na kutekeleza miradi ya kimkakati.

“Huu ni mradi utakaoondoa tatizo la maji na tuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa kama hii kwa sababu maji ni muhimu na kila mwananchi anapaswa kutumia maji yaliyo safi na salama,”amesema Luteni Mwambashi

“Huu ni mwendelezo wa mradi mkubwa na tumeona uliwekwa jiwe la Msingi na Kiongozi wa Mwenge 2019  na tumepitia nyaraka mbalimbali na tumepewa taarifa kuwa tayari wateja 4700 wanapata huduma na maunganisho bado yanaendelea na kwa sababu hiyo Mbio za Mwenge wa Uhuru  Kitaifa 2021 tumejiridhisha kwa asilimia 100,” ameongezea.

Aidha, katika kusisitiza zaidi amewataka wananchi waendelee kutunza miundo mbinu ya miradi na kutokuihujumu ili mamlaka ziendelee kusambaza maji.

Akisoma taarifa ya Mradi huo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ritamary Lwabulinda amesema  mradi wa Pugu-Gongo la Mboto umejielekeza katika kuondoa tatizo la maji kwenye maeneo ya Pugu hadi Tabata Kinyerezi.

Ritamary amesema, mradi wa Pugu -Gongo la Mboto  umezaliwa kutoka Mradi mkubwa wa maji wa Kibamba-Kisarawe  na ulianza ujenzi Juni 2019 na kumalizika April 2021.

Amesema, gharama  za mradi huu ni Bilion 7.3 bila VAT na gharama zote za mradi huo ni makusanyo ya huduma za majisafi na Usafi wa Mazingira.

“Katika mradi huu, ulihusisha bomba kuu la kusafirisha maji kutoka Kisarawe hadi Ukonga kwa urefu wa Km 13.5 na ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji kwa umbali wa km 50 kwa ukubwa wa mabomba ya inchi 3 hadi inchi 8,” amesema

“Bomba kuu litakuwa na uwezo wa kusafirisha kiwango cha maji kipatachi lita Milion 2.8  kwa siku,”amesema

Amesema, utekelezaji wa asilimia 100 ambapo utekelezaji wake umefanyika kwenye upimaji wa njia ya mabomba, usanifu wa mradi, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa tanki , ujenzi wa uzio eneo la tanki na ofisi ya kihuduma DAWASA Ukonga.

Mradi huo unasambaza maji kwa wakazi zaidi ya 450,000 katika maeneo ya Pugu, Majohe, Gongo la Mboto, Bangulo, Ukonga -Airwing, Kigogo na Sehemu ya Kinyamwezi  na Buyuni Chanika.

Mkandarasi wa mradi huo ni kampuni ya CHICO kutoka China na Mhandisi Mshauri ni Kampuni ya WAPCOS kutoka India.

No comments :

Post a Comment