Thursday, August 19, 2021

BILIONI 39 KUKAMILISHA MRADI WA KUBORESHA VYUO VYA UALIMU NCHINI

Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mouguso Nathanael Hinju,akitoa taarifa ya Chuo kwa waandishi wa habari waliofika katika chuo hicho kuhusu Ujenzi na Ukarabati wa Chuo uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mshauri Elekezi Mhandisi Renatus Dominick ,akielezea jinsi walivyojipanga kukamilisha kwa wakati Ujenzi na Ukarabati wa vyuo mbalimbali unaosimamiwa na  Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu Mkoani Mbeya wakiwa kwenye chumba cha maabara iliyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso Osiana Kitomari,akiipongeza  Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kufanya ukarabati pamoja na ujenzi katika Chuo hicho na kikifanya kuwa bora kutokana na mazingira ya sasa.

Muonekano wa Bweni la Wavulana lililopo katika Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu Mkoani Mbeya lililojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

 

Muonekano wa nyumba za walimu zilizopo katika Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu Mkoani Mbeya yaliyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

 

Muonekano wa majengo ya Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu Mkoani Mbeya yanayojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.

Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mouguso Nathanael Hinju,akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari waliofika katika Chuo hicho kukagua na kujionea ukarabati na ujenzi katika chuo hicho uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

…………………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Tukuyu

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada zinatumia bilioni

39  kukamilisha mradi wa kuboresha Vyuo vya Ualimu nchini unaoitwa ‘Upgrading Teachers Colleges UTC’ katika Vyuo vinne vya Mpuguso, Shinyanga, Kitangali na Ndala ifikapo Juni 2022.

Hayo yamesemwa na Mshauri Elekezi wa UTC, Mhandisi Renatus Dominick wakati akizungumza na  wandishi wa habari waliofika katika Chuo Cha Mpuguso kilichopo Tukuyu Mkoani Mbeya, amesema kiasi kinachotumika kukamilisha mradi huo  ni Sh Bilioni 39 ambazo Serikali ya Tanzania inatoa Sh Bilioni 8.2 huku Canada wenyewe wakitoa Sh Bilioni 30.

Amesema kuwa Mradi huo wa UTC ambao ulianza Mwaka 2016 unatekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizi mbili ambao umelenga kufanya maboresho katika miundombinu ya Vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kukarabati majengo yaliyokuepo na kujenga mengine mapya.

” Huu mradi unaitwa The Upgrading Teachers Colleges UTC ulianza mwaka 2016 kwenye vyuo hivi vinne vya Ualimu Nchini na tunarajia kukamilisha Juni 2022, lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira ya vyuo hivi ambavyo vingi ni vyuo vya zamani ambavyo tayari majengo yake yalishachakaa, mpaka sasa tumeshapokea kiasi cha Sh Bilioni 29 kutoka Serikali ya Canada kwa ajili ya mradi huu,” Amesema Mhandisi Renatus.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hiko cha Mpuguso, Nathaniel Hinju ameishukuru Serikali kwa kuwezesha kufanyika kwa maboresho hayo ambayo ameeleza kuwa yatakua na faida kubwa ikiwemo kuboreka kwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kutokana na uwepo wa maabara, maktaba na madarasa mengine mapya.

“Zipo faida nyingi za maboresho ya mradi huu, ulinzi na usalama umeimarika kutokana na kupata umeme wa Sola, ongezeko la matanki ya kuhifadhia maji, uwepo wa ukumbi umetoa fursa kubwa ya kufanya mabaraza ya chuo kwa ufanisi zaidi pamoja na wanafunzi kunufaika kusoma masomo ya Sayansi kwa vitendo,” Amesema Hinju.

Amesema sababu zilizopelekea kuomba mradi huo ni uchakavu na upungufu wa miundombinu kutotosheleza kufuatana na mahitaji, ongezeko la udahili wa wanachuo uliotokana na matokeo mazuri ya mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari MMES na maoni ya chuo kuendesha kozi za Sayansi

Bw.Hinju amesema ujenzi na ukarabati wa Chuo hicho ulianza mwaka 2016 na ulihusika katika ujenzi wa nyumba nne za watumishi, tatu zikiwa za ghorofa moja zenye uwezo wa kuishi watumishi 13, ujenzi wa mabweni mawili yenye ghorofa moja moja yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 304, ukumbi wa mikutano na ukarabati wa nyumba nne za watumishi.

Mradi huo pia umegusa ujenzi wa majengo mawili ya madarasa yenye ghorofa moja moja ambapo madarasa hayo yana uwezo wa kuchukua wanachuo 720, jengo la mhadhara, maabara, maktaba na ukarabati wa mabweni mawili na choo cha wasichana.

” Tunaishukuru sana Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuboresha mazingira yetu ya kufundishia na kujifunzia,” Amesema Hinju.

Nae Mwanafunzi wa Chuo hicho Osiana Kitomari ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa maboresho hayo ambayo yataongeza chachu ya wao kuzidi kujisomea lakini pia kufungua mwanya kwa Chuo kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi na hivyo kuongeza uzalishaji wa idadi kubwa ya Walimu nchini.

No comments :

Post a Comment