Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu akifungua kikao maalum cha uundaji wa Baraza la wazee Mkoa wa Ruvuma na kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaoliongoza baraza hilo ngazi ya Mkoa.
******************
WAZEE wa Mkoa wa Ruvuma wamefanya kikao maalum cha uundaji Baraza la Wazee la Mkoa
kilichofanyika kwenye ukumbi wa mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.Waliochaguliwa kuunda Baraza hilo kwenye uchaguzi ulishirikisha wawakilishi kutoka wilaya za Nyasa,Mbinga,Songea,Tunduru na Namtumbo ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa amechaguliwa Elenzian Nyoni kutoka Manispaa ya Songea.
Wengine waliochaguliwa ni Lusiana Nduguru kutoka Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambaye amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti,Katibu ni Winfrid Mbilinyi kutoka Halmashauri ya Madaba na Naibu Katibu Philipo Katyale kutoka Halmashauri ya Songea.
Viongozi wengine waliochaguliwa kuunda Baraza la Wazee wa Mkoa ni Mtunza Hazina amechaguliwa Esta Nzuyu kutoka Halmashauri ya Mji wa Mbinga,Mwakilishi wa wanaume Yustin Mande kutoka Halmashauri ya Nyasa na Mwakilishi wa wanawake amechaguliwa Maria Luoga kutoka Manispaa ya Songea.
Akizungumza wakati anafungua kikao cha uchaguzi huo,mgeni
rasmi Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bakari Ally Mketo
amesema Taifa linawategemea sana wazee ambao ni hazina kubwa katika
jamii.
Taifa bila wazee halina dira,wala muelekeo,sehemu yeyote panapokosekana wazee,pana hatari ya kuangamia,alisisitiza Mketo.
Amesema vijana wana mengi ya kujifunza kutoka kwa wazee kwa sababu wazee wanafahamu siri kubwa na hekima ya kuwa kiongozi bora ambapo amesisitiza kuwa Taifa linawategemea wazee ndiyo maana yanaundwa mabaraza ya wazee katika ngazi mbalimbali.
Amesema serikali imetoa nguvu kubwa katika mabaraza ya wazee na kwamba busara ya wazee kwenye mabaraza hayo itasaidia kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 29,2021
No comments :
Post a Comment