************************
TUME ya Utumishi wa Umma inawakumbusha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kuwasilisha Tume, taarifa zao kwa wakati za masuala ya kiutumishi kwa
kila robo (miezi mitatu) ya mwaka wa fedha husika, ikizingatiwa kuwa uwasilishaji wa taarifa hizi Tume ya Utumishi wa Umma kuhusu masuala ya kiutumishi katika Utumishi wa Umma si jambo la hiari, bali ni takwa la kisheria.Bwana Lamech Mapunda, Mchumi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma amesema haya mwishoni mwa wiki wakati wa kupokea na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kiutendaji za kiutumishi kutoka kwa watumishi wa umma na wadau wa Tume wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea kufanyika.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 (2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019), Tume ya Utumishi wa Umma imepewa Mamlaka ya kuwataka Waajiri na Taasisi mbalimbali katika Utumishi wa Umma kuwasilisha taarifa kuhusu uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu. Taarifa hizi ni chanzo kimojawapo kinachotumika kuonesha hali ya Utumishi wa Umma Nchini” alisema Mapunda.
Bwana Mapunda, alisema tathmini ya hali ya uwasilishaji wa taarifa kutoka kwa Waajiri na Taasisi za Umma inaonesha kuwa baadhi ya Taasisi zilizopaswa kuwasilisha taarifa Tume ya Utumishi wa Umma, hazikutekeleza takwa hilo la kisheria kwa kipindi husika na nyingine ziliwasilisha baada ya muda kupita.
“Kupitia Maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika, Tume inawakumbusha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kuwasilisha Taarifa zao kwa wakati ikizingatiwa kuwa uawasilishaji wa Taarifa za masuala ya kiutumishi si jambo la hiari, bali ni takwa la kisheria” alisema Bwana Mapunda.
Bwana Lamech Mapunda alisema kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu yanayoendelea kufanyika, Tume itapokea changamoto za kiutendaji za kiutumishi na kuzitafutia ufumbuzi. Hivyo, Tume tunawakaribisha Watumishi wa Umma na Wadau kufika katika Ofisi yetu ya Tume ya Utumishi wa Umma, iliyopo mtaa wa Luthuli, Jijini Dar es Salaam kuanzia kesho Jumatatu tarehe 21 hadi 23 Juni, 2021.
No comments :
Post a Comment