Saturday, June 19, 2021

THBUB KUTOA MAFUNZO YA HAKI ZA BINADAMU KWA WATUMISHI WA AFYA 500

*************************

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), idara huru ya Serikali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyo kitovu cha ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini hivi

karibuni inatarajia kuendesha mafunzo ya siku mbili ya haki za binadamu na utawala bora kwa zaidi ya watumishi 500 wa sekta ya afya.

Lengo la kuendesha mafunzo hayo ni kukuza uelewa wa watumishi wa sekta ya afya kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kuyafikia matarajio yao.

Katika awamu hii ya kwanza Mafunzo hayo yatawahusisha watumishi walioko katika hospitali 11 zilizoko katika mikoa sita (6) ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, na yanatarajiwa kutolewa kuanzia Juni 17 mpaka 25 mwaka huu.

Mikoa na hospitali zitakazohusika katika mafunzo hayo ni: Dodoma (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa); Dar es Salaam (Hospitali ya Amana, Temeke na Mwananyamala); Mwanza (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Sekou toure, Hospitali ya Wilaya Ilemela na Nyamagana); na Lindi (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Sokoine).

Kwa upande wa Zanzibar mafunzo yatafanyika Unguja (Hospitali ya Mnazi Mmoja) na Pemba (Hospitali ya Wilaya ya Wete na Chakechake). Katika utekelezaji wa kazi hii ofisi zote sita (6) za Tume zilizoko katika mikoa tajwa zitahusika.

Mafunzo hayo yatatolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa THBUB wa miaka mitano (2018/2019 – 2022/2023); ambao moja ya malengo yake ni kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora. Utoaji wa mafunzo ya haki za binadamu na utawala kwa makundi mbalimbali ya watanzania ni mojawapo ya njia ya kufikia lengo hilo.

Huko nyuma Tume imewahi kutoa mafunzo kama haya kwa viongozi na watendaji wa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria nchini – Jeshi la Polisi, Magereza na Mahakama. Aidha, imekuwa ikitoa mafunzo haya kwa watendaji wa Serikali za Mitaa, walimu na wanafunzi wa takriban ngazi zote.

Kazi zinazofanywa na watumishi wa sekta ya afya zina uhusiano wa moja kwa moja na haki za binadamu. Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Ibara ya 12 na 14; na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 11 na 13. Vifungu hivyo vinazungumzia kuhusu usawa, heshima kwa utu wa mtu na haki ya kuishi.

Katika muktadha huo huo, kwa mujibu wa katiba zote mbili, huduma zinazotolewa na Serikali na taasisi zake mbalimbali zinatakiwa zikidhi misingi ya haki za binadamu na ziwawezeshe wananchi kufaidika na huduma hizo.

Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na taarifa nyingine mbalimbali kumekuwepo na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu wananchi kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na baadhi ya watumishi katika baadhi ya vituo vya afya nchini. Malalamiko hayo yameambatana na madai ya uwepo wa upendeleo, lugha mbaya na rushwa, kutaja bali kwa uchache.

Kwa misingi hiyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeamua kuendesha mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora kwa watendaji wa sekta ya afya kote nchini.

Tume inaamini kuwa mafunzo haya yatawawezesha watumishi wa sekta ya afya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora na wananchi watafurahia huduma zinazotolewa.

Pia, watumishi wa sekta ya afya watakaopata mafunzo haya wanaweze kuelimisha wananchi mifumo sahihi ya kutoa taarifa na kudai haki zao wanapohisi kuwa zimevujwa au kukiukwa kwa misingi ya utawala bora.

Zaidi ya hayo, elimu hii ni hatua moja mujarabu ya kuifikia ndoto ya Tume ya kuwa na jamii yenye kuheshimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora, na utu wa mtu.

 

No comments :

Post a Comment