Tuesday, June 8, 2021

RAIS SAMIA AITAKA WIZARA YA AFYA KUWEKA UTARATIBU MZURI WA UCHUKUAJI MAITI ZENYE MADENI

Na.Alex Sonna,Dodoma 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ameiagiza wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweka utaratibu mzuri ambao hautaleta usumbufu wa uchukuaji wa maiti zenye madeni hospitalini
Rais Samia ametoa agizo hilo leo Juni 8,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa niaba ya wanawake wote nchi.
Amesema  kuwa utaratibu wa sasa ambao umekuwa ukizuia kutoa maiti hospitalini kwa kigezo cha kulipa gharama za matibabu kabla ya kifo si mzuri.
“Nakuaguza waziri uweke utaratibu mzuri wa ulipaji wa gharama za matibabu wakati wa matibabu yakiendelea ili kuondoa changamoto za kuzuia maiti kwa kigezo Cha kudaiwa gharama hizo,”amesma Rais Samia.
 Aidha amesema kuwa moja ya Mipango mizuri ni kutoa gharama za matibabu kabla ya mgonjwa kufariki sio hadi mgonjwa afariki ndio wapewe taarifa alisema kuwa haifai bali waweke Mpango mzuri sio kuzuia maiti.
” Nawapongeza wanawake wote waliojitokeza kufika kwenye mkutano huu, wengine mmesafiri kutoka mbali, na wengine wakifuatilia kupitia vyombo mbalimbali vya habari, nawashukuru na wanaume waliojumuika nasi hapa na wale wanaotufuatilia kupitia vyombo vya habari,”amesema Rais 
Rais Samia amewashukuru wanawake wa Tanzania kwa ushirikiano wanaompa tangu alipopata dhamana ya kuliongoza Taifa la Tanzania kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
“Kupitia wanawake wa Dodoma nazungumza na Taifa lote, nimejiwekea utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali nchini kwa makusudi ya kubadilishana mawazo na kusikia kutoka kwao vile ambavyo wangependa tundelee,”amefafanua Rais Samia.
“Ikumbukwe kwamba nimeshakutana na viongozi wa dini hapa Dodoma, wazee  wa mkoa Dar es Salaam, viongozi wa sekta binafsi, pia nitazungumza na vijana mkoani Mwanza kwa niaba ya vijana wote nchini na leo ni zamu ya wanawake,”amesema  Rais.
Naye  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima amesema kuwa Wanawake wanatoa mchango muhimu sana katika maendeleo ya nchi na katika nyanja mbalimbali. 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewashukuru wote kwa kushiriki katika mkutano huo, wageni ,wadau,wadhamini na wote mliofika na kumuhakikishia Mhe. Rais kuwa Mkoa wa Dodoma ni shwari na salama.

 

No comments :

Post a Comment