Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa 3 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bungeni jijini Dodoma, Juni 30, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utaratibu wa utoaji wa vibali vya ukaazi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki umesaidia kupunguza hatua za kuchakata maombi kutoka siku 33 za hadi saba.
Amesema kuwa kwa
sasa waombaji hawalazimiki kwenda katika Ofisi za Kazi kwa sababu
taarifa zote zinapatikana kwenye mfumo na watajaza fomu moja tu ambayo
huwa na taarifa zote za kazi na ukaazi tofauti na awali ambapo
wawekezaji walilazimika kujaza fomu mbili.
Ameyasema hayo leo
(Jumatano, Juni 30, 2021) wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Bunge la
12, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 31 mwaka
huu.
Amesema miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kupitia
matumizi ya mfumo huo ni kupungua kwa siku za kushughulikia maombi ya
vibali vya kazi kutoka siku 14 hadi siku tatu. “Hali hii, pamoja na
mambo mengine, imesaidia kupunguza malalamiko ya kuchelewa kupata majibu
ya maombi ya vibali vya kazi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa watumiaji wa mfumo kwa
ajili ya maboresho na tayari imeshakutana na kupokea maoni ya wadau wa
ndani na nje kikiwemo Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Waajiri (ATE),
Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Taasisi ya Sekta Binafsi na
kuyajumuisha maoni hayo kwenye maboresho.
Amesema Serikali
inakamilisha maboresho ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Sura 436)
kwa kuainisha maeneo yaliyokuwa na changamoto za kiutendaji na kuathiri
jitihada za kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini. Mfumo huo
unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti mwaka huu.
“Sambamba na
marekebisho hayo ya sharia, tangu tarehe 23 Aprili, 2021 tumeanza
kutumia mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya
kazi kwa raia wa kigeni na katika hatua za majaribio tayari maombi zaidi
ya 500 yameshughulikiwa kupitia mfumo huo.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha bajeti ya 2021/2022 inatoa matokeo
yaliyokusudiwa, Serikali itaimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki
kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji na hivyo kudhibiti matumizi
ya fedha za umma kwa kuepuka malipo hewa na manunuzi ya umma ya bidhaa
na huduma zisizokidhi viwango vya ubora.
Amesema Serikali
itahakikisha uwepo wa thamani halisi ya matumizi ya fedha za umma
katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki
tena kwa wakati pale inapobaini ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni
za matumizi ya fedha za umma.
“Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2021/2022 unakwenda sambamba na Mikakati ya Serikali
katika kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, utendaji na
uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wote wa sekta ya umma. Hatua hizo,
zinalenga kuhakikisha bajeti hii inatoa matokeo yaliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watendaji wa Serikali
hususan wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) wajipange vema na wahakikishe suala la posho za madaraka kwa
watendaji wa kata na vijiji kupitia mpango wa halmashauri linasimamiwa
na kutekelezwa ipasavyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka
watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanatenga maeneo
maalumu kwa ajili ya vijana na wafanyabiashara wadogo sambamba na
kuwapatia elimu pamoja na kuwashirikisha katika kubaini maeneo
yanayoendana na biashara zao. Amewaagiza watendaji hao wasikilize na
kushughulikia kero za wananchi kwa wakati ikiwa ni pamoja na kutenga
siku maalum kwa ajili hiyo.
No comments :
Post a Comment