Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuiunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ina nia thabiti ya
kuwaletea maendeleo.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu Juni 7, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Nandagala, Likunja, Nambilanje na Ruangwa Mjini mkoa wa Lindi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imetoa Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari katika kata ya Likunja ambayo itakuwa ni kubwa kuliko zote wilayani Ruangwa.
Aliongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na madarasa 13, matundu ya vyoo 30, jengo la utawala , maabara 2 kubwa, mabweni 4, nyumba za walimu 2, bwalo na jiko “pia vitajengwa viwanja vya michezo katika shule hiyo”.
Amesema Wilaya ya Ruangwa imedhamiria kuhakikisha inajenga shule za sekondari katika kata ambazo hazina shule hizo lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata fursa ya kusoma.
Kuhusu huduma ya maji safi na salama, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeanza kufanya usanifu wa mradi wa maji kutoka eneo la Ndanda ambako kuna chanzo kikubwa cha maji cha Mbwinji ili kuyafikisha Ruangwa.
Amesema kuwa mradi huo utavinufaisha vijiji vya Mbecha, Michenga, Chimbira A na B, Nandagala, Namahema, Mpumbe, Nkowe, Mitoke na Likunja.
Akizungumzia sekta ya umeme, Waziri Mkuu amesema kazi ya usambazaji umeme vijijini na maeneo yaliyopo nje ya miji inaendeleavizuri na wale wote ambao wamelipia gharama za kuunganishiwa umeme wataunganishwa kupitia mpango wa REA.
Ameagiza kwamba vijiji vyote ambavyo havijapatiwa na huduma ya umeme viunganishwe kwa kuwa mkandarasi amekwishapatikana.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wananchi kuanza kujenga maboma ya ujenzi wa zahanati na yeye Mbunge wao atasaidia upatikanaji wa mabati.
Kadhalika amesema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa inakusudia kujenga Chuo cha Afya ambacho kitatoa mafunzo ya Uuguzi na wahudumu wengine wa sekta ya afya lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalamu wa afya.
Waziri Mkuu Juni 8, 2021 anatarajia kufungua mashindano ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari (UMISETA) katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
No comments :
Post a Comment