Tuesday, June 29, 2021

Biteko Azindua ‘NMB Mining Club’

 

Waziri wa Madini - Dotto Biteko (kushoto) na Afisa Mkuu wa Mikopo Benki ya NMB – Daniel Mbotto wakizindua rasmi jukwaa la ‘NMB Mining Club’ katika hafla ya uzinduzi iliofanyika katika hoteli ya Morena - Dodoma.
 

Baadhi ya wadau wa Sekta ya Madini kutoka Kanda ya Kati katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa NMB Mining Club uliofanyika Jijini Dodoma.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara Benki ya NMB – Alex Mgeni akiwaelimisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini Kanda ya Kati waliohudhuria uzinduzi wa NMB Mining Club kuhusu huduma na bidhaa zinazotolewa na benki ya NMB.

 Benki ya NMB imeendelea kuweka historia nyingine tena kwa kuzindua jukwaa la kwanza nchini mahsusi la kuwahudumia wadau wa Sekta ya Madini liitwalo ‘NMB Mining Club’.

Klabu hiyo mpya imejumuisha zaidi ya wadau wa madini 200 wa Kanda ya Kati na imelenga kutoa mafunzo kuhusu maarifa ya biashara (elimu juu ya mipangilio ya biashara na elimu ya mwendelezo wa kitaalamu wa madini) na fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu wa kibiashara.

Wadau hao ni pamoja na wamiliki wa migodi, maduka makubwa ya vifaa vya uchimbaji, viongozi kutoka kampuni za madini, Kampuni ya Taifa ya Madini (Stamico), vyama vya wachimbaji wa kada zote na madalali.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa jukwaa hilo uliofanyikakatika hoteli ya Morena- Dodoma, Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko aliwapongeza NMB kwa ubunifu huo wa kuwafikia na kuwaunganisha wadau wa Sekta hiyo huku wakiwapa fursa ya mafunzo ya biashara na kubadilishana mawazo kwa ajili ya ufanisi wao binafsi na kisekta kwa ujumla.

Mhe.Biteko, amewahakikishia wawekezaji na wadau wengine wa sekta ya madini mazingira bora ya uwekezaji na kufanya biashara akisema hicho ni kitu muhimu kwa ustawi wa sekta hiyo na maendelo ya taifa kwa ujumla.

Awali, Afisa Mkuu wa Mikopo wa NMB, Bw. Daniel Mbotto, alisema mafunzo hayo yamekuja wakati biashara nyingi zikipata changamoto akitolea mfano wa kushuka kwa thamani ya bei ya Tanzanite kwenye soko la dunia.

Kuhusu “NMB Mining Club”, Bw. Mbotto alisema ni mpango unaolenga kufikia miji sita nchini yaani Mwanza, Chunya, Morogoro na Arusha, ukianzia Dodoma na Kahama na maeneo ya karibu kwa lengo la uwezeshaji na kutoa mafunzo ya biashara. Ubunifu huu ndio unaoifanya NMB kuendelea kuwa kinara wa huduma na bidhaa katika sekta ya kibenki.

No comments :

Post a Comment