Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii leo Jijini Dodoma ambapo amesema shughuli za Uhifadhi zinakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo baadhi ya Wananchi na Viongozi kugeuza mashamba katika maeneo ya Wanyamapori hali inayosababisha migogoro ya binadamu na Wanyamapori kuongezeka kila siku hali inayotishia usalama wa Uhifadhi pamoja na maisha ya Wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi.
…………………………………………………………………………………
Wizara ya Maliasili na Utalii inakusudia kunyanga’nya maeneo yote ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii ambayo yatakutwa yamelimwa ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na
Wanyamapori wakali na Waharibifu .Hatua hiyo inakuja kufuatia
baadhi ya wananchi na viongozi kufanya mashamba na kuanza kulima mazao
ya chakula katika Hifadhi hizo hali inayopelekea Wanyamapori kama tembo
kuacha kula nyasi na kulazimika kutoka nje ya Hifadhi na kwenda kula
mazao hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo leo mapema Jijini Dodoma wakati
akizungumza na Watendaji wa Wizara hiyo kuhusu changamoto zinazoikabili
sekta ya Uhifadhi nchini hususan kwa Wananchi wanaoishi kando kando mwa
maeneo yaliyohifadhiwa.
Amesema kwa mujibu wa sheria
maeneo hayo ni mali ya vijiji na yanasimamiwa na Serikali za Vijiji
husika na mapato yatokanayo na Hifadhi hizo za Jamii hutumiwa kwa ajili
ya manufaa ya Wananchi ikiwemo kuboresha huduma za kijamii kama vile
shule na zahanati.
Amesema maeneo hayo ya uhifadhi
kusimamiwa na Serikali za vijiji ni ushirikishwaji wa Jamii wa moja kwa
moja ili kuiwezesha Jamii kufaidikana uhifadhi wa moja kwa moja
Amesema hatua hiyo ya
kunyang’anya itakwenda sambamba na upandishaji hadhi wa Jumuiya hizo za
Hifadhi za Wanyamapori za Jamii na kuwa Mapori Tengefu ( Game Controled
Area) ambayo kwa mujibu wa Sheria Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
(TAWA) ndiye atakayepewa kusimamia maeneo hayo.
Akizungumzia hatua hiyo ya
kunyang’anya Usimamizi kutoka Serikali za Vijiji na kupelekwa TAWA, Dkt.
Ndumbaro amesema kutatuma ujumbe mzito kwa Serikali za Vijiji ambazo
zinazosimamia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori hizo kuwa zimepewa
jukumu la kusimamia Uhifadhi na sio vinginevyo.
Waziri Dkt. Ndumbaro amesema
kuna jumla ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori zipatazo 22 na kati ya
hizo ni Jumuiya za Wanyama[pori 10 pekee ndizo zinafanya vizuri
kimapato na kiuhifadhi.
Kufuatia hali hiyo, amewataka
Wakuu wa wilaya nchini ambao ndio Wenyeviti wa Jumuiya za Hifadhi za
Wanyamapori nchini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kupiga vita
shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo hayo ambazo
haziendani na Uhifadhi.
” Nina taarifa ya baadhi ya
Jumuiya hizo za Uhifadhi kuna Wakuu wa wilaya ambao ni Wenyeviti wa
kusimamia maeneo hayo nao wanalima katika maeneo, hadi kuna wengine
wameamua kufungua mashamba ya minazi katika maeneo ya Wanyamapori hili
halikubaliki” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Amesema kuna baadhi ya Jumuiya
za Hifadhi za Jamii za Wanyamapori zinazofanya vizuri na zimekuwa
zikikusanya pesa nyingi kutoka kwa Watalii ikiwemo Jumuiya ya Hifadhi ya
Wanyamapori ya Jamii ya Ikona ambayo kwa mwaka inapata bil. 2.6
zinazogawanywa kwa vijiji vitano pekee.
Ametoa wito kwa Serikali za
Vijiji kuhakikisha zinasimamia ipasavyo Uhifadhi katika maeneo hayo kwa
vile maeneo hayo ni utajiri mkubwa endapo kama yatasimamiwa kwa ajili ya
utalii na sio kugeuza kuwa mashamba.
No comments :
Post a Comment