Thursday, May 6, 2021

WIZARA YA ELIMU YAZINDUA MKATABA WA HUDUMA KWA WATEJA, NAIBU WAZIRI KIPANGA ASISITIZA UWAJIBIKAJI

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo kitabu cha mkataba wa huduma kwa wateja uliozinduliwa leo jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja leo jijini Dodoma.
Watendaji, Watumishi wa Wizara ya Elimu na wadau wa wizara hiyo wakimfuatilia Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja jijini Dodoma leo.

Charles James, Michuzi TV

WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imezindua rasmi mkataba wa

huduma kwa wateja huku ikiwataka watendaji na watumishi wa wizara hiyo kufuata ahadi iliyowekwa kwenye mkataba huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba huo, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema mtumishi yeyote ambaye ataenda kinyume na mkataba huo atachukuliwa hatua na ambao watafanya vizuri watapongezwa.

Naibu Waziri Kipanga pia ameziagiza taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Elimu na Vyuo Vikuu vyote kuhakikisha zinakua na mikataba iliyo hai na wasio na mikataba hiyo waharakishe kuwa nayo huku pia akiwataka wale ambao wana mikataba iliyopitwa na wakati waiboreshe.

Madhumuni ya mkataba huo ni kuboresha mahusiano baina ya wizara na wateja wao lakini pia ukikusudia kuongeza uelewa kuhusu aina na ubora wa huduma zinazotolewa, haki na wajibu wa wateja na jinsi wanavyoweza kuwasiliana.

" Mkataba wa huduma kwa wateja ni makubaliano kati yetu watoa huduma na wateja wetu ikiwa ni ahadi ya kutoa huduma bora kwa wateja, mkataba huu unaelekeza na kuainisha viwango vya huduma ambavyo wateja wetu wanatarajia kupata ili kufikia malengo yao.

Aidha mkataba huu unaelekeza na kutoa fursa kwa umma kuwasilisha maoni kuhusiana na ubora wa huduma zetu na kutoa mrejesho ama malalamiko endapo huduma tunazozitoa hazitakidhi haja na matarajio ya wateja wetu," Amesema Naibu Waziri Kipanga.

Naibu Waziri Kipanga amewaagiza watendaji na watumishi wote walio chini ya Wizara ya Elimu kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuzingatia taaluma zao katika kutekeleza mkataba huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo amesema mkataba huo umeainisha aina ya wateja inaoenda kuwahudumia lakini pia utakuza mahusiano ya wizara na wateja wake.

" Nitoe rai kwa watumishi wenzangu kutoa huduma kwa weledi na ubora, tusiwahudumie wananchi wetu kwa kuangalia sura zao bali kwa kufuata taratibu zetu za kazi, " Amesema Dk Akwilapo.

 

No comments :

Post a Comment