Monday, May 31, 2021

WATU MILIONI 6 HUFA KILA MWAKA KWA UVUTAJI WA MOSHI WA SIGARA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza tamko la serikali kupiga vita uvutaji wa sigara katika ukumbi wa (JKCI) Muhimbili jijini Dar es salaam leo.

TAKRIBANI watu milioni sita hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku na

bidhaa zake zikiwemo sigara na shisha au kuvuta moshi kutoka kwa mvutaji huku kati kati yao ni watoto ambao hupoteza maisha kwa asilimia 28, wanawake asilimia 6 na wanaume asilimia 12, huku ikikadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2030 vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku vitaongezeka na kufikia zaidi ya milioni nane kwa mwaka.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya siku ya kutotumia tumbaku duniani yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo amesema katika maadhimisho hayo ya Mei 31 dunia huadhimisha siku hiyo kwa kuelimisha dunia madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa njia mbalimbali ikiwemo kunusa, kuvuta au kutafuna.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni Dhamiria Kuacha Kutumia Tumbaku na Bidhaa zake.” Kauli mbiu hii imelenga kuhamasisha kuacha matumizi ya tumbaku kwa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na uhusiano uliopo baina ya matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Kauli mbiu hii inahimiza kuwepo kwa mpango na hatua za Serikali na jamii ili kupunguza visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza kutokana na tumbaku.” Amesema.

Gwajima amesema, Licha ya watu laki sita kupoteza maisha kila mwaka kwa kutumia tumbaku na kuvuta moshi kutoka kwa mtumiaji madhara yanayowapata waathirika ni pamoja na kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani, magonjwa ya njia ya hewa, mapafu na kisukari na mengineyo ambayo huathiri moyo, mishipa ya damu na kuongeza uhatarishi wa kupata shinikizo la juu la damu.

”Pia tumbaku hupunguza kiwango cha oksijeni inayoweza kusafirishwa na damu na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kuifanya damu kuganda na kusababisha magonjwa mengine ya moyo ambayo huweza kupelekea kiharusi au kifo cha ghafla….Tuwalinde watoto tumeona asilimia 28 ya watoto hupoteza maisha kwa kuathirika na moshi kutoka kwa wavutaji tunajenga taifa la watoto imara ni wajibu wetu kuwalinda, Wizara kwa kushirikiana na Serikali na jamii tunapaswa kuhamasika na bila kushurutisha katika kuacha matumizi ya tumbaku na bidhaa zake.” Amesema.

Amesema malengo katika maadhimisho ya mwaka huu ni kuhamasisha kuamua kwa dhati kuachana na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ili kuilinda jamii kutokana na madhara ya kiafya yatokanayo na tumbaku, kuongeza uelewa kwenye kundi kubwa la jamii juu ya madhara yanayoweza kupatikana kutokana na kutumia tumbaku au kuwa karibu na mtu anayetumia tumbaku pamoja na kuipa moyo nchi katika kuongeza nguvu kwenye utekelezaji wa mkataba wa kimataifa na kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku ili kuilinda jamii dhidi ya athari za matumizi ya tumbaku na bidhaa zake pamoja na kuepuka gharama kubwa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza.

Kuhusu mkakati wa Serikali ya Tanzania katika suala hilo Dkt. Gwajima amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa sera ya Afya ya 2007 inayolenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukizwa kwa umahiri zaidi kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO,) ambalo limekuwa likifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku na hadi sasa Serikali ya Tanzania inaendelea kusisitiza kuaacha utumiaji wa bidhaa za tumbaku iitwayo ‘Shisha.’

Madhara yatokanayo na tumbaku na bidhaa zake hayawezi kudhibitiwa kwa Serikali pekee jamii hasa vijana na taasisi zisizo za kiserikali kutoa ushirikiano na kuhakikisha harakati imepewa wito kwa kushiriki kikamilifu kwa kupokea elimu inayotolewa.

 

No comments :

Post a Comment