*******************************
Taasisi ya Mama Alaska Jamii kwa kushirikiana na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Trade Mark East Africa, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na Ofisi ya
Mbunge wa Jimbo la Karagwe, wamezindua semina yenye lengo la kutoa elimu ya biashara, kutambua sheria za kufanya biashara mipakani na kuzitambua fursa mbalimbali za biashara kwa wanawake wajasiriamali wa wilaya Karagwe.
Semina hiyo imezinduliwa leo Mei 17, 2021 katika ukumbi wa Tripple P, Omurushaka Karagwe Kagera na itatolewa kwa kata zote 23 za wilaya ya Karagwe kwa kuwafikia wanawake wajasiriamali 300 ambao ni wawakilishi wa vikundi wanaotegemewa kupeleka elimu hii kwenye vikundi vyao ili kuwafikia wajasiriamali zaidi ya 4,000 wa Karagwe ili kuleta tija kwenye Biashara zao.
Wakati akifungua Semina hiyo, Afisa biashara mkoa wa Kagera, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Issaya Tendegu amewataka wanawake wajasiriamali wa wilaya ya Karagwe kulima kilimo chenye tija kwa kutumia mbegu bora ambazo zinaongeza thamani ya mazao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, Bw. Issaya Tendegu amezitaja fursa nyingi za kibiashara zilizopo wilaya ya Karagwe na kutoa ufafanuzi wa fursa kubwa ya kijiografia ya Karagwe kuwa moja kati ya wilaya iliyopo mpakani mwa Tanzania na nchi nyingine za jirani kama Uganda, Rwanda na Burundi.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Mama Alaska Jamii, Bi. Jennifer Bashungwa, ameeleza semina itakavyowasaidia akina mama wajasiliamali kutambua na kufahamu sheria za kufanya biashara mipakani zitakazowasaidia kunufaika na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kupitia semina hizi za biashara, wanawake wajasiliamali wa wilaya ya karagwe watajengewa uwezo na uelewa wa kukuza biashara na kutambua fursa za masoko yaliyowazunguka.
Taasisi ya Mama Alaska Jamii imekua ikitoa mafunzo ya biashara kwa makundi mbalimbali ya wajasiliamali wakiwemo Mama Lishe wa Mkoa wa Dar es salaam na wakulima wa zao la mpunga wa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
No comments :
Post a Comment