Imeelezwa kuwa, Fedha za ufadhili huo zitatumika katika hifadhi za Serengeti, Nyerere na pamoja na Selous na ufadhili huo umekuja baada ya dunia kukumbwa na janga la Corona (Covid-19,) ambalo limeathiri sekta ya utalii kwa kushusha mapato katika maeneo ya hifadhi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili imeelezwa kuwa Balozi Hess amesema, ufadhili huo utasaidia katika shughuli za hifadhi na utanufaisha Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA,) Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) kama nguzo ya kupandisha mapato baada ya idadi ya watalii kupungua na mradi huo unaitwa 'Ufadhili wa Dharura Katika Kuhifadhi Bioanuwai ya Tanzania.'
Imeelezwa kuwa Ujerumani ni moja kati ya washirika muhimu kwa Tanzania hasa katika masula ya uhifadhi wa Bioanuwai pamoja na hifadhi na hiyo ni kutokana na mizizi imara ya urafiki iliyojengwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Prof. Bernhard Grizmek aliyekuwa Rais wa Ujerumani.
Mwaka huu Tanzania na Ujerumani zinasherehekea miaka 60 ya mahusiano bora baina ya nchi hizo hasa katika uhifadhi ambapo Ujerumani imetumia zaidi ya shilingi bilioni 300 (zaidi ya Euro milioni 106) kwa miaka mitano iliyopita katika kuhifadhi asili na wanyamapori Tanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania Dkt. Damas Ndumbaro kwa niaba ya Serikali ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa ufadhili huo na kueleza kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kuyapa nguvu maeneo muhimu ya hifadhi za Serengeti na Nyerere.
Amesema, ufadhili huo utatoa msaada kwa TANAPA na TAWA kwa kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Ndumbaro amesema Serikali imejizatiti katika kuendeleza juhudi za kuhifadhi Bioanuwai na wataendelea kufuata nyayo za Serikali ya Ujerumani kwa juhudi zake za kuhakikisha wanyamapori pamoja na hifadhi zinatunzwa kwa kizazi cha sasa na baadaye.
No comments :
Post a Comment