Thursday, May 6, 2021

RUGEMALIRA AIOMBA MAHAKAMA IMFUTIE KESI, 'BARGAINING' HAINA MUAFAKA


Mfanyabiashara , James Rugemalira, Seth na Makandege wakitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu leo mara baada ya kesi yao kuhairishwa  kesi ya Uhujumu Uchumi.

ALIYE kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL na Mfanyabiashara, James Rugemalira ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imfutie mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili pamoja na wenzake wawili kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kukamilisha upelelezi kwa muda wa miaka minne.

Katika kesi hiyo  mbali na Rugemalira wanashtakiwa wengine ni mmiliki wa IPTL, Herbinder Seth na wakili wa kujitegemea Joseph Makandege.

leo Mei 6, 2021 Ombi hilo la limewasilishwa na Wakili wake, Ngalo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia upelelezi kama umekamilika ama la na pia kujua muelekep wa mazunguzo ya kumaliza kesi baina ya DPP, Seth na Makandege ulipofikia ambao mwaka jana waliandika barua kwa DPP kuonesha nia ya kukiri makosa yao ( bargaining)

Wakili Ngalo akisaidiana na John Chuma wamedai kuwa mteja wao (Rugemalira) ameomba mashtaka dhidi yake yafutwe kutokana na kucheleweshwa kwa upelelezi, kwani wapo ndani tokea mwaka 2017, na kwamba Mahakama inaweza kutumia mamlaka yake kufuta kesi hiyo.

Ngalo amedai kuwa Kila kesi hii ikija mahakamani upande wa mashtaka wanakuja na taarifa kuwa upelelezi haujakamilika na mazungumzo yanaendelea, huku wakieleza kwamba Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo...., "Tunaomba hii dhana ifike mwisho mshtakiwa amekaa gerezani tangu mwaka 2017 kwa kisingizio kwamba upelelezi haujakamilika, ni upelelezi gani huu wa miaka minne?." 

Aidha, mshtakiwa watatu (Makandege) katika kesi hiyo, ameieleza mahakama kuwa, ameondoa nia yake ya kuingia makubaliano na DPP ili kukiri makosa hayo kutoka na kwamba mazungumzo hayo hayana afya na yamechukua muda mrefu kukamilika.

Wakili wa utetezi wa Makandege, Alex Balomi amedai mahakamani hapo kwamba mteja wake ameiondoa nia ya kufanya makubaliano na DPP ya kumaliza kesi kutoka na kuzungushwa zungushwa bila mafanikio yoyote.

Naye, Wakili anayemtetea Seth, Dorah Mallaba amedai kuwa mteja wangu wake amemuarifu kuwa Ofisi ya DPP haijamtembelea mahabusu kama walivyokuwa wamemuahidi kwa ili wafanye mazungumzo ya kumaliza kesi.

" Mheshimiwa, tunaomba upande wa mashtaka useme unaomba muda gani wakuweza kukamilisha mazungumzo hayo kama hawawezi basi upelelezi ukamilike ili waweze kusikiliza kesi." Amedai Wakili Mallaba.

"Jambo lipo wazi kesi imechukua muda mwingi kukamilika kwa upelelezi, Mahakama ilishatoa amri mbalimbali kutokana na maombi kama haya.

"Ni kweli kesi hii ni ya uhujumu uchumi bila hati za DPP haiwezi kusikilizwa katika Mahakama hii. Mahakama ina mamlaka, lakini kama sheria inakataza haiwezi kutoa uamuzi, haina maana kwamba DPP au upande wa mashtaka kutumia mamlaka kwa kutokutekeleza wajibu wake.

Tunapopewa hizi ofisi tuzitumie, tufanye kazi kama sheria inavyoturuhusu, jambo ambalo hatupendi kufanyiwa wewe usimfanyie mwenzio, hii dunia iliyoundwa na Mungu hakuna jambo jema au baya utakalofanya usipewe zawadi, tunapopewa kazi tufanye kwa haki."  Hakimu Shaidi amesema mara baada ya kusikiliza hoja na Malalamiko hayo.

Kesi imeahirishwa hadi Mei 20, 2021 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia upelelezi kama umekalika au la, washtakiwa wamerudishwa rumande.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

 

No comments :

Post a Comment