Monday, May 31, 2021

RAIS SAMIA AUNGWA MKONO NA EALA


Na Woinde Shizza , Michuzi Tv ARUSHA

BUNGE la jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA,) limejipanga kumpongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi pekee Afrika Mashariki mwanamke ambaye ameonyesha mwelekeo mzuri katika kusimamia

demokrasia katika uongozi wake.

Wakizungumza  mwishoni mwa wiki  katika bunge  la nne linalofanyika makao makuu ya jumuiya hiyo Jijini Arusha, wabunge kutoka Tanzania Dkt. Abdulah Makame,  Adam Kimbisa na Mariam Ussi  walisema bunge hilo limepanga kutoa mwaliko maalumu  kwa Rais Samia ili afike katika bunge hilo waweze kumpongeza na kutoa nasaha zake.

Kimbisa ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge wa EALA kutoka Tanzania alisema kiu ya wabunge wa bunge hilo ni  kuona Rais huyo akisimamia vema Demokrasia katika uongozi wake na bunge hilo limejipanga kumwalika Rais Samia kuja kulihutubia ili kupata mwelekeo wake katika mtangamano wa jumuiya hiyo.

Kwa upande wake mbunge Ussi Yahaya amesema kuwa bunge hilo la Afrika mashariki limeamua kumpongeza kwa dhati Rais Samia na lipo tayari kufanya naye kazi katika kuijenga jumuiya hiyo.

"Hii Ni hatua nzuri ambayo wabunge tumeweke hoja ya kumpongeza rasmi Rais Samia ambapo wabunge wengi wameunga mkono na dhamira hiyo inasubiriwa kupitishwa na spika wa bunge hilo Martin Ngoga." Alisema Ussi.

Aliongeza kuwa pamoja na hatua hiyo ya bunge la EALA wao Kama wabunge wa wanawake kutoka Tanzania wanakusudia kumwalika kwa lengo la kumpongeza.

Naye Dkt Abdulah Makame alisema kuwa bunge hilo limeunga mkono hoja iliyotolewa ya kumpongeza Rais Samia na kuadhimia aalikwe na kulihutubia bunge hilo ili kutoa mawazo yake kuhusu masuala ya mtangamano wa jumuiya hiyo.

Katika hatua nyingine Dkt Makame amewasilisha hoja binafsi ya kutaka bunge hilo liwe na bendera yake inayojitegemea ili kuweza kushushwa nusu mringoti pindi  kutatokea majanga mbalimbali ikiwemo  mbunge kufariki kama sehemu ya kutoa heshima ya kumuenzi marehemu.

Alisema hoja hiyo imepitishwa na bunge hilo na kinachosubiriwa ni kikao kijacho ili aweze kuwasilisha mswada huo ili wabunge waweze kuujadili na hatimaye kuipitisha kama kanuni na sheria ya bunge hilo kutumia bendera yake.

"Bunge lilikuwa likijadili hoja mbalimbali ikiwemo hoja ya marekebisho ya Sheria ya Afrika Mashariki inayohusiana na nembo za Afrika Mashariki ikiwemo bendera"

"Nimepata kibali cha kwenda kuandaa hiyo sheria na kabla ya mwisho wa mwaka 2021 huo mswada huo utatinga bungeni uweze kujadiliwa"alisema Makame.

 

No comments :

Post a Comment