
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza na waandishi
wa habari wakati wa kutangaza kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa 26 wa
Wanahisa wa Benki hiyo unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi Mei 22,
2021, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Kila
mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa
ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au
kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki. Kulia ni
Mkurugeni wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa na
kulia ni Katibu wa Kampuni Benki ya CRDB, John Rugambo.
===== ==== ====
Benki
ya CRDB inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa siku ya
Jumamosi tarehe 22/05/2021 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mkutano huo unafanyika
kufuatana na Sheria ya Makampuni (Companies Act) namba 212 ya mwaka
2002, ambapo kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo
unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki.

Akizungumzia
katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya
Mount Meru Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid
Nsekela amesema ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki
mkutano huu muhimu, Benki ya CRDB imeandaa utaratibu kwa wanahisa ambao
kwa namna moja au nyingine hawatoweza kufika Arusha waweze kushiriki
mkutano wa kwa njia za kidigitali.
“Kwa
kuzingatia uzoefu tulioupata kwa kufanya mkutano wa 25 kwa njia ya
mtandao, wanahisa walipitisha pia azimio la mkutano wa 26 kufanyika kwa
njia zote mbili kwa maana ya kuruhusu wanahisa wanaoweza kushiriki kwa
kufika Arusha lakini pia kuruhusu wanahisa wanaoweza kushiriki kwa njia
ya mtandao kutumia njia hiyo ambapo itakua ni historia kwa mkutano mkuu
wetu kufanyika nama hii” alisema Nsekela.
Mkutano
Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utatanguliwa na semina maalum
kwa wanahisa yake ili kukuza uelewa wa masuala mbalimbali ya fedha na
uwekezaji katika masoko ya mitaji. Semina hiyo itafanyika siku ya Ijumaa
tarehe 21/05/2022 kuanzia saa 3 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC). Mgeni Rasmi katika semina hiyo anatarajiwa
kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mh. Mwigulu Nchemba ambapo mada
mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wa masuala ya fedha, sheria na
uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Kwa
mujibu wa Nsekela hii itakua ni mara ya kwanza kwa Mkutano wa Mkuu wa
Wanahisa wa Benki ya CRDB kufanyika kwa njia zote mbili ambapo mkutano
wa mwaka jana ulikuwa wa kwanza kwa Benki kutumia njia za kidigitali ili
kukabiliana na changamoto ya COVID-19. Zaidi ya wanahisa 1400 waliweza
kushiriki mkutano wa mwaka jana idadi ambayo haijawahi kufikiwa katika
mikutano ya kawaida ambayo hufanyika jijini Arusha kwa miaka yote.
“Nachukua
fursa hii kuwakaribisha wanahisa wote katika semina na mkutano mkuu na
niwahakikishie wanahisa wote ambao watashiriki kwa njia ya mtandao kuwa
tumejipanga vizuri katika kuhakikisha kila wanashiriki kama wanahisa
ambao watakua AICC na tumeweka maelezo katika tovuti yetu ya Benki (www.crdbbank.co.tz) ya jinsi gani wanaweza kushiriki hatua kwa hatua” aliongeza Nsekela.
Pamoja
na mambo mengine yatakayojadiliwa katika mkutano mkuu huo ikiwemo
maboresho ya katiba ya kampuni, shauku kubwa kwa wanahisa ni kufahamu
juu ya pendekezo la gawio kwa wanahisa kwa mwaka uliopita ukizingatia
kuwa Benki ya CRDB imeendelea kupata matokeo mazuri sokoni ambapo katika
hesabu za mwaka wa fedha ulioisha Benki iliweza kupata faida kabla ya
kodi ya Shilingi Bilioni 236 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kutoka
Shilingi Bilioni 175 iliyopatikana mwaka 2019.




No comments :
Post a Comment