Thursday, May 6, 2021

BALOZI WA DENMARK WAIPATIA FCS FEDHA ZA NYONGEZA KIASI CHA FEDHA ZA DENMARK KRONE MIL.4.3


Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) wakikabidhiana hati za mkataba wa fedha ya ruzuku ya nyongeza Sh. Bilioni 1.6 kutoka Denmark kwaajili ya kuisaidia FCS kuweza kutekeleza miradi ya Asasi za Kiraia Chini.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) akiweka saini wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa Sh Bilioni 1.6 kutoka Ubalozi wa Denmark kwaajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ya Asasi za kiraia nchini Tanzania.
Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga (kulia) wakionesha mkataba waliosaini mara baada ya kumalizika kwa zoezi hilo katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga   (wa nne kulia),  Menejimenti ya FCS na Afisa wa DANIDA mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kutia saini mkataba wa fedha za Kitanzania Sh Bilioni 1.6 kutoka ubalozi wa Denmark katika Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.. 
*******************************
Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania umeipatia Foundation for Civil Society (FCS) fedha za nyongeza kiasi cha fedha za Denmark Krone milioni 4.3 sawa na fedha za Kitanzania Sh bilioni 1.6 kwa lengo la kuchangia maendeleo endelevu nchini Tanzania.
Fedha hizi za nyongeza zinaleta jumla ya Sh bilioni 4.4 fedha za ufadhili wa Ubalozi wa Denmark nchini kwa asasi ya kiraia kwa muhula wa mwaka 2021.
Ubalozi, kupitia Shirika la Maendeleo la kimataifa DANIDA, umesaini makubaliano ya kuongeza Msaada wa Denmark kwa FCS tarehe 5 Mei 2021. 
Mkataba huo umesainiwa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Nørgaard Dissing- Spandet na Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga.
Balozi ameeleza sababu za ubalozi wa Denmark kushirikiana na asasi za kiraia hususan FCS  “Tunafanya kazi kwa kushirikiana na asasi za kiraia, kwa sababu tunaamini kwamba, asasi za kiraia ni kiini katika kuhakikisha mamilioni ya Watu wanakua, wanawezeshwa kimaendeleo, mamilioni ya wasichana na Wanawake, na watu wenye ulemavu wanakuwa na uwezo wa kupaza sauti zao katika jamii na kusikika, kuwa na uwezo wa kushiriki katika maisha ya kisiasa, kiuchumi na namna ya kuitambua jamii inayowazunguka na umuhimu wa Utamaduni wake.
 
Hivyo tumependezwa na tunajivunia kwamba, leo tumetia saini ya Mkataba mpya wa nyongeza ya jumla ya kiasi cha fedha za kidenmark (Danish Krone) milioni 4.3 Sawa na shilingi bilioni 1.6 fedha za kitanzania.
 
Kiasi hiki tunatarajia kitumike vyema katika kuzifikia asasi za kiraia takribani 130 za kitanzania kwa misingi chanya ya kuhamasisha Utawala kidemokrasia, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuboresha maisha ya Watanzania wengi”. Alisema Mhe. Balozi Mette Nørgaard Dissing- Spandet
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga alisema kuwa Denmark imekuwa ikisaidia jitihada za FCS kuboresha Maisha ya Mamilioni ya Watanzania hasa jamii katika ngazi za vijijini na makundi ya pembezoni.
 
Akizungumzia juu ya ufadhili wa ziada uliopokelewa, Bwana kiwanga alibainisha kuwa FCS inatarajia kuongeza mafanikio zaidi kwa wananchi kupitia kazi zake.
 
“Sasa tuko kwenye kipindi cha mpito kutoka kukamilika kwa mpangomkakati wa 2016 – 2020 miaka hiyo tuliweza kufikia zaidi ya wanachi milioni 5 nchi nzima katika juhudi za kuwawezesha wananchi kushawishi utawala wa kidemokrasia na unaojumuisha watu wote. kwa mfano, miradi yetu ya uwajibikaji Jamii imewawezesha wananchi kufuatilia miradi ya umma ipatayo 945 yenye thamani ya takribani Tsh bilioni 312. Programu zetu za uwezeshaji kiuchumi zimechangia katika Manispaa kadhaa nchini kutoa Tsh. Milioni 406 kama mikopo kusaidia shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu na vijana. kupitia programu hii pia tumechangia katika vijana kupata Tsh bilioni 6.34 kama mikopo ya halmashauri.
 
“Pia tumewezesha wananchi kuripoti visa 8,887 vya ukatili wa kijinsia (GBV) na hivyo kusaidia kupatikana  kwa haki za maelfu ya wanawake na wasichana nchini. Miradi yetu ya haki za ardhi pia imewezesha zaidi ya wanawake 3,400 kote nchini kupata hati zao za kimila za umiliki wa zaidi ya ekali 4,575 za ardhi zenye makisio ya thamani takriban Tsh bilioni 17.
 
“Fedha hizi za nyongeza zitasaidia sana kuhakikisha tunadumisha jitihada zilizoleta mafanikio kwa jamii, kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza tija ya kazi zetu tunapojitahidi kutoa mchango mkubwa wa kujenga Tanzania tunayoitaka” Alisema.
Tangu mwaka 2017 hadi mwaka huu wa 2021 Ubalozi wa Denmark kupitia shirika lake la maendeleo DANIDA limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 15.5 kwa asasi ya kiraia ya FCS.

 

No comments :

Post a Comment