Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ kufuatia kuwepo kwa wafanyakazi hewa na kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Serikali, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Waliotenguliwa
ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi
la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad pamoja na Mkuu wa
Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Comodore Hassan Mussa
Mzee.
Akitoa
taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya Habari Ikulu Jijini
Zanzibar,Dk. Mwinyi alisema kuwa kufuatia taarifa za uwepo wa
wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ, aliumda Kamati ya Uchunguzi
kwa kufanya uhakiki wa idadi ya wafanyakazi pamoja na viwango vya
mishahara vinavyotolewa kwa vikosi vyote.
Alisema
kuwa ripoti ya Kamati ya Uhakiki iliyomfikia ilieleza kwamba kulikuwa
na wafanyakazi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika
utaratibu unaotakiwa ikiwa na maana kwamba walikuwa watumishi hewa.
Alisema
kwamba fedha zilikuwa zikipokelewa na kutumika katika kipindi chote
hicho ambapo walikuwa katika vikosi hivyo na kueleza kwamba
lililothibitika ni kwamba wakati Kamati imeanza kazi zake baadhi ya
vikosi kikiwemo JKU walianza kutengeneza utaratibu wa kurasimisha uwepo
wa wafanyakazi hao hewa.
Alisema
kwamba waliwahi kukamatwa baadhi ya Maafisa katika nyumba ya mtu
binafsi wakiwa wamewafisha sare za Jeshi vijana na kuwapiga picha ili
kuthibitisha kwamba wamo katika ajira rasmi.
Rais
Dk. Mwinyi alisema kwamba imebainika kuwa fedha zilizotumika kwa
upotevu ni kiasi cha TZS bilioni 2,235,725,000.00 kutokana na fedha
zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hewa.
Vile
vile, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Kamati ilikwenda kuhakiki ulipaji
wa posho katika vikosi hivyo ambapo ilibaini wastani wa upotevu wa fedha
zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya posho kwa mwezi wa Disemba ni jumla
ya TZS milioni 304,135,939.00 sawa na wastani wa TZS bilioni
1,824,815,634.00 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Disemba.
Alisema
kwamba Kamati haikuishia hapo na iliendelea kubaini kwamba kuna
watumishi ambao walikuwa wameshastaafu lakini bado walikuwa wakiendelea
kupokea mishahara ambapo kuliwa na wastaafu 12 wa Idara Maalum za SMZ
waliokuwa wakiendelea kulipwa mishahara baada ya kustaafu ambapo ni
kinyume na utaratibu.
Alieleza
kwamba hali hiyo imesababishwa na wahasibu wakuu wa Idara Maalum za SMZ
kwa uzembe ama kwa kukusudia ambapo kwa misingi hiyo Serikali imeingia
hasara ya jumla ya TZS milioni 44,610,280.00.
Hata
hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wastaafu wawili waliitwa na Kamati
na kuhojiwa na baadae walikubali kurejesha fedha jumla ya TZS milioni
10,766,560.00 fedha ambazo ziliingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali.
Alisema
kwamba hayo yote yanabainisha kuwa ni kweli kulikuwa kuna watumishi
wameshastaafu na bado walikuwa wakilipwa mishahara kinyume na utaratibu.
Rais
Dk. Mwinyi alisema kwamba mtumishi anapofukuzwa kazi hutakiwa kuwekewa
kizuizi cha mishahara mara tu anapofukuzwa kazi hata hivyo, Kamati
imegundua kwamba wahasibu wakuu wa vikosi pamoja na waingizaji wa
taarifa za mishahara huchelewesha mchakato huo kwa makusudi ili fedha
hizo zitumike katika matumizi yao binafsi.
Hivyo,
Kamati imegundua kwamba wahasibu huwatengenezea madeni watumishi
waliokuwa wamefukuzwa kazi na fedha hizo hukatwa na kupelekwa kwenye
duka la kikosi na hatimae fedha hizo huingia mifukoni mwa wahasibu hao
ambapo jumla ya fedha zilizopotea kwa aina hiyo ni kiasi cha TZS
117,724,000.00.
Aidha,
alisema kuwa Kamati imebaini kwamba kuna ukataji wa Posho ya chakula
kwa askari Kapera kinyume na utaratibu kwani kwa kawaida askari
anapojiriwa hukaa Kambini kwa kipindi cha miaka miwili na kukatwa posho
ya chakula ya kiasi cha TZS 70,000 kwa kila askari kwa kila mwezi fedha
ambazo ni kwa ajili ya kujikimu.
Alisema
kwamba kwa upande wa JKU Kamati imebaini kwamba jumla ya askari 771
walikatwa fedha za posho ya chakula bila ya kukaa Kambini na fedha zao
kuingia mifukoni mwa watu wachache kiasi cha TZS 539,700,000.00 kwa
kipindi cha miezi kumi kuanzia mwezi wa Machi 2020 hadi Disemba 2020.
Pia,
Kamati hiyo imebaini kwamba Maafisa na askari wananyimwa fursa ya
kupata vielelezo vya taarifa za mishara yao ikiwemo Payslip zao hiyo
imepelekea kwa baadhi ya askari hao kukatwa mishahara yao kinyume na
utaratibu na kutokujua malengo ya makato hayo.
Alisema
kuwa Kamati hiyo pia, imegundua kuwa kuna baadhi ya Askari waliokuwa
wakitiliwa posho na kukatwa kwa kuingizwa kwenye maduka ya vikosi hali
ambayo iliibua malalamiko mengi kwa askari na kuwakosesha morali ya
kufanya kazi.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa takriban askari wote walikiri
kuwa kwa mara ya kwanza baada ya kuanza uhakiki huo ndipo wamepewa
Payslip zao pamoja na kujua stahiki zao.
Hivyo,
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa pamoja na Kamati kufanya kazi nyingi na
kugundua udhaifu sehemu nyingi sana inatosha kwa hayo yaliobainika
kuweza kuchukua hatua za kisheria ambapo aliagiza wahasibu na waingizaji
wa data wachukuliwe hatua za kisheria na tayari wameshasimamishwa kazi
na utaratibu wa kuchukuliwa hatua za kisheria unaendelea.
No comments :
Post a Comment