Friday, April 30, 2021

RAIA SABA WA IRAN KIZIMBANI MKOANI LINDI


Raia saba wa Iran walokamatwa Aprili 23,2021 mkoani Lindi akisafirisha dawa za kulevya.

Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv
RAIA saba wa Iran wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi wa wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine na Methamphetamine zenye uzito wa jumla ya kilo 859.36

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Joseph Maugo akisaidiana na wakili Mwandamizi Juma Maige imewataja washtakiwa hao kuwa ni,

Jan Mohammad Miran, Issa Baluchi Ahmad, Amir Hussein Kasom, Salim Baluchi Fedhmuhammad, Ikbal Pakil Mohammad, Mustapha Nowan Kadir Barkshi na Jawid Nuhanur Nur Mohammad.

Kesi hiyo ya uhujumu namba 02 ya 2021 imesomwa leo Aprili 30,2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Maria Bantulayne.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Maugo amedai, Aprili 23, 2021 huko katika Bahari ya Hindi mkoa wa Lindi ndani ya eneo la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Herione zenye uzito wa kilo 504.36.

Imeendelea kudaiwa kuwa siku na mahali hapo, washtakiwa hao pia walikamatwawa wakisafirisha dawa zingine za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 355 kinyume cha sheria.

Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya Uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Mei 14 2021 washtakiwa wamerudishwa rumande.
Boti waliyoitumia Raia saba wa Iran walokamatwa Aprili 23,2021 mkoani Lindi wakisafirisha dawa za kulevya.

 

No comments :

Post a Comment