Friday, April 9, 2021

MFUKO WA PAMOJA WA SACCOS WAZINDULIWA


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akizindua Mfuko wa Pamoja wa SACCOS kukopeshana kwa kukata utepe wa vijitabu vya Sera mbalimbali za Mfuko huo, Jijini Dar es salaam.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na Wanaushirika wakati wa Uzinduzi wa Mfuko wa Pamoja wa SACCOS kukopesha (Central Financing Facility) Mkoani Dar es salaam

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania SCCULT (1992) Ltd Dkt. Gervas Machimu akieleza namna Mfuko wa Pamoja wa SACCOS utakavyosaidia kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo.
 

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amekitaka Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania SCCULT (1992) kuwa

wabunifu katika kubuni bidhaa zenye manufaaa kwa Vyama Wanachama ili kuonesha na kutoa fursa ya wanachama wa SACCOS kupata mikopo nafuu itakayosaidia kuondoa umasikini na kukuza Uchumi wa Taifa.

Mrajis ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Uzinduzi wa Mfuko wa Pamoja wa SACCOS kukopeshana Central Financing Facility (CFF) uliofanyika Aprili 09, 2021 Mkoani Dar es salaam.

Akizindua Mfuko huo Mrajis ameitaka SCCULT kubuni bidhaa mbalimbali za mikopo itakayoendana na mahitaji ya wanachama wa SACCOS pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA katika uendeshaji na utunzaji mzuri wa taarifa za Wanachama.

“Ni lazima bidhaa zitazofaa wanaushirika ili waone faida na thamani ya kukopa ndani ya Mfuko unaoundwa na SACCOS zetu kwa lengo la kuhakikisha Chombo chetu cha SCCULT kinaimarika na kuwezesha SACCOS kusaidia Wanachama wengi zaidi,” alisema Dkt. Ndiege

Aidha, Mrajis Alisisitiza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali ina wajibu wa kulinda maslahi ya wanaushirika. Hivyo, haitosita kuchukua hatua endapo yeyote atakiuka Sheria, Kanuni na taratibu za Ushirika zilizowekwa kwakuwa Ushirika ni Sekta mtambuka inayogusa Uchumi na maisha ya watu.

Akielezea malengo ya Mfuko huo Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania SCCULT (1992) Ltd Dkt. Gervas Machimu alibainisha kuwa Mfuko wa CFF ni muungano wa nguvu za kifedha za SACCOS wanachama ambao unatoa fursa kwa SACCOS hizo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha pindi SACCOS inapokuwa na changamoto za Kifedha kwaajili ya kutoa huduma kwa wanachama wake hususani mikopo.

Katika uzinduzi huo Dkt. Machimu ameeleza SCCULT tayari imepata kiasi cha Fedha cha Shillingi Millioni 270 kutoka kwa Wadau wa Ushirika ambayo itatumika kukopesha (SACCOS) ili kuhakikisha vyama hivyo vinakuwa na ukwasi wa kutosha kuweza kukopesha wanachama wake. Akiongeza kwa kutoa rai kwa SACCOS na Wadau wengine kujitokeza kuendelea kuchangia Mfuko huo kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa SACCOS.

Aidha Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa SACCOS zitakazokopeshwa fedha hizo ni zile ambazo ni wanachama wa SCCULT na ambazo zitakazo kuwa ni sehemu ya Mfuko huo kwa kuweka Akiba na kujisajili na Mfuko wa CFF. Akiongeza kuwa ili kuhakikisha Mfuko huo unakuwa na usimamizi imara tayari kuna masharti yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sera za Mfuko zilizoandaliwa.

“Vyama vitakavyokopa katika Mfuko huo ni vile ambavyo vimepata Leseni ya Usimamizi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Vyama vilivyokakuguliwa, vilivyo na Ukomo wa Madeni yanayopitishwa na Mrajis wa Ushirika,” alisema Dkt. Machimu

Dkt. Machimu alifafanua zaidi kuwa Mikopo itakayoanza kutolewa ni ile ya itakayofuata taratibu za kupungua salio la usawa (reducing balance) kwa kiasi cha 10%, akieleza kuwa SACCOS zitakazopata mkopo zitatoa mikopo hiyo kwa riba isiyozidi 17%.

No comments :

Post a Comment