Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kazi ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere wilayani Rufiji, Aprili 10, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wajenzi wakati alipokagua kazi ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere wilayani Rufiji, Aprili 10, 2021. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua kazi ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere wilayani Rufiji, Aprili 10, 2021. Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na kushoto ni Mhandisi Mkazi wa Mradi, John Mageni.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa fedha za kugharamia mradi wa umeme wa maji ya Mto Rufiji (RHPP) ili ukamilike kwa wakati.Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Aprili 10, 2021) baada ya kukagua mwenendo wa mradi huo unatarajiwa kukamilika June 2022. Amesema kuwa Serikali itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.
Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kazi nzuri yenye viwango na ubora wa hali ya juu inayofanywa na Kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na ile ya Elsewedy Electric zote kutoka nchini Misri chini ya usimamizi wa TANESCO, TANROADS na Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha Watanzania kupata umeme mwingi na wa gharama nafuu ambao utasambazwa nchini kote na ziada kuuzwa nje ya nchi ili kulipatia Taifa fedha za kigeni.
Waziri Mkuu amesema bwawa hilo linatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 ambazo zikijumlishwa na megawati 1,500 zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali nchini hivi sasa zitaifanya Tanzania kuwa na umeme utakaotosheleza mahitaji yake na ziada kuuzwa kwa majirani.
”Lengo la kuanzisha mradi huu ni moja ya juhudi za Serikali za kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwa sababu uzalishaji wake ni wa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine. Uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa kutumia maji inagharimu shilingi 36 hadi shilingi 50 huku umeme unaotumia vyanzo vya mafuta uniti moja inazalishwa kwa gharama ya shilingi 440 hadi shilingi 600.”
Amesema faida nyingine ya ujenzi wa mradi huo ni pamoja na kuzalisha ajira kwa Watanzania mbalimbali wanaoshiriki katika kuujenga na kutoa huduma mbalimbali kama wauzaji wa vifaa vya ujenzi, mafuta, vyakula na huduma nyingine zinazohitajika kwenye mradi huo.
Waziri Mkuu amesema tayari TANESCO imeshatangaza zabuni ya ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka kwenye chanzo cha mradi huo hadi Chalinze mkoani Pwani na ukifika Chalinze njia moja itakwenda Dar es Salaam na nyingine Dodoma ili kuwezesha umeme huo kusambazwa nchi nzima.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Nishati ifuatilie changamoto zote zinazoweza kukwamisha ujenzi wa mradi huo ili kuzipatia ufumbuzi na ihakikishe unakamilika kwa wakati. Pia amewataka wananchi wanaozunguka mradi huo kutoa ushirikiano kwa wajenzi kwa kuwahakikishia usalama wao, mali zao na vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo.
Mapema, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato ameishukuru Serikali kwa kuwa wakati wote tangu kuanza kwa mradi huo hadi sasa imeendelea kutoa fedha za kugharamia mradi huo kwa wakati na tayari imeshatoa zaidi ya shilingi trilioni mbili. Hadi kukamilika mradi huo utagharimu shilingi trilioni 6.5.
No comments :
Post a Comment