Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, akiangalia dhahabu
iliyosafishwa kufikia kiwango cha 999.9 (purity) wakati alipotembelea
kiwanda cha Mwanza Precious Minerals Limited. Kushoto kwake ni Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Bw. Venance
Mwasse.
Benki
Kuu ya Tanzania imelipongesha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa
hatua iliyofikia ya kuanza usafishaji wa dhahabu hapa nchini kwa ...ubora
wa kimataifa.
Pongezi
hizo zimetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens
Luoga, wakati alipotembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza
Precious Minerals Limited, kilichopo jijini Mwanza Ijumaa na kujionea
maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa, ikiwemo kuanza uzalishaji.
“Haya
ni mapinduzi makubwa katika sekta ya madini na ukombozi kwa wachimbaji,
wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta hii. Ndoto ya Tanzania kuacha
kusafirisha dhahabu ghafi naona inaelekea kutimia”, alisema Gavana
Luoga.
Aidha,
Prof. Luoga alivutiwa na taarifa kwamba kiwanda hicho ambacho
kinamilikiwa kwa ubia kati ya serikali kupitia STAMICO na wawekezaji wa
nje, pia kina uwezo wa kutenganisha dhahabu na madini mengine ambayo
yana thamani katika masoko ya madini duniani.
“Kwa
uwezo wa kiwanda hiki, nina imani mtaweza kununua dhahabu yote nchini
na nchi jirani na kwa kuwa dhahabu inayotoka kiwandani hapa itakuwa na
nembo ya Tanzania, itaitangaza nchi kimataifa” alisema Gavana wa Benki
Kuu.
Katika
kiwanda hicho, STAMICO inamiliki asilimia 25 wakati asilimia zilizobaki
75 zinamilikiwa kwa pamoja na kampuni za ROZZELA General LLC ya Dubai,
Umoja wa Walme za Kiarabu (UAE) na ACME Consultant Engineers PTE Limited
ya Singapore (RGTACE).
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alimweleza Gavana
Luoga kuwa “katika ubia huu, hisa za STAMICO zitakuwa zinaongezeka kwa
asilimia tano (5), ambapo baada ya miaka 15 STAMICO itakuwa imefikisha
asilimia 51 na wabia wengine kubaki na asilimia 49.
Alieleza
pia kwamba katika ubia huo, STAMICO itakuwa inapata asilimia 2.5 ya
mauzo ghafi kwa huduma za usimamizi (Management fee) zinazotolewa na
Kampuni”.
Kiwanda
hicho kimeanza uzalishaliji wa majaribio tarehe 21 Aprili 2021. Kina
uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa ubora wa kimataifa
(999.9 purity) ni kitakuwa kimojawapo cha viwanda vikubwa vya kusafisha
dhahabu barani Afrika.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO alieleza kuwa faida za uwekezaji huo ni
nyingi zikiwemo kuchangia mapato ya nchi kupitia ada za ukaguzi,
kuongeza mapato ya halmashauri kupitia tozo mbalimbali, ajira,
teknolojia ya kisasa ya kuchakata dhahabu na kupunguza utoroshaji wa
dhahabu inayochimbwa Tanzania.
Aidha,
kupitia kiwanda hicho, dhahabu ya Tanzania itatambulika kupitia nembo
yake maalum ya uasili (originality mark), madini mengine yataweza
kuainishwa na kuthaminishwa hapa nchini na kuiwezesha Benki Kuu kuanza
kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria za nchi.
Gavana
Luoga ambaye aliambatana na wataalam mbalimbali wa Benki Kuu,
aliwaeleza umuhimu wa kuwa na hati ya utambuzi ya kimataifa
(accreditation) ili kuiwezesha Benki Kuu kununua dhahabu hiyo kama
sehemu ya akiba ya fedha za kigeni za nchi (foreign reserves).
Kiwanda
hiki kimejengwa kimkakati kikiwa katikati ya mikoa izalishayo dhahabu
kwa wingi kama Geita, Mara, Shinyanga na Mwanza yenyewe. Kiwanda
kinategemea kitakua kinapata dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo,
wachimbaji wakubwa wenye migodi hapa nchini, dhahabu zilizotaifishwa na
serikali, dhahabu kutoka nchi jirani na dhahabu kutoka kwa madalali
(dealers).
Uwekezaji
huo, siyo tu utaongeza mapato yatokanayo na madini, bali pia utaipa
heshima nchi ya Tanzania kwa kuwa usafishaji wa dhahabu utakuwa wa
viwango vya kimataifa.
No comments :
Post a Comment